Jul 22, 2021 07:57 UTC
  • Rouhani: Iran na Uturuki ni madola mawili makubwa ya Ulimwengu wa Kiislamu

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo ya simu na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki na mbali na kumpa mkono wa Idi, yeye, serikali na wananchi wa Uturuki amesema kuwa, nchi hizi mbili ni madola makubwa katika eneo hili na kwenye Ulimwengu wa Kiislamu na zina nafasi muhimu katika utatuzi wa matatizo ya eneo hili zima.

Mazungumzo hayo ya simu yalifanyika jana ambapo Rais Rouhani alisema pia kuwa, inafurahisha kuona kuwa leo hii kuna uhusiano mzuri baina ya Tehran na Ankara katika nyuga zote; za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kimataifa.

Vile vile ametilia mkazo udharura wa kuendelezwa ushirikiano huo katika siku za usoni na kuimarishwa zaidi akisisitiza kuwa, Iran na Uturuki zinashirikiana pia katika masuala tofauti ya kimataifa na kikanda yakiwemo ya kutatua matatizo yanayoukumba Ulimwengu wa Kiislamu.

Amesema, nchi zote mbili zinalichukulia suala la kutatua matatizo ya mataifa ya Kiislamu kuwa ni jukumu lake linalowajibisha nchi hizi mbili kushirikiana zaidi na zaidi.

Bendera za Iran na Uturuki

 

Ameendelea kusisitizia msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine yoyote na kuhimiza kutatuliwaa matatizo yanayojitokeza kwa njia ya mazungumzo.

Kwa upande wake, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki naye ametoa mkono wa Idi kwa serikali na wananchi wa Iran na kusema kuwa, uhusiano wa mataifa haya mawili ndugu ya Kiislamu ni mkubwa, wa kupendana na unaozidi kuimarika siku baada ya siku. 

Ameshukuru juhudi za Rais Rouhani za kuhakikisha uhusiano wa Tehran na Ankara unastawi zaidi na zaidi  na kuelezea matumaini yake ya kuona hali hiyo inaendelea pia katika serikali ijayo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags