Kujihami kutakatifuu, siri na ufunguo wa kushinda njama zote za adui
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kumbukumbu za wapiganaji wa Kiislamu katika kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu na familia zao ni hazina kubwa isiyo na mbadala na rasilimali ya taifa la Iran.
Ayatullah Ali Khamenei aliyasema hayo alasiri ya jana katika hadhara ya makamanda, wanajeshi, walemavu wa vita na wasaani na kuongeza kuwa, kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu kinaonesha picha ya hali ya mlingano wa nguvu katika dunia ya utawala wa ubeberu. Ameongeza kuwa: Kuna udharura wa kuwafikishia walimwengu ujumbe wa imani na jihadi na ujumbe wa kutoshindwa taifa la Iran kupitia njia ya kuanzisha harakati ya kutarjumu na kufasiri athari za kimaandishi na kuonesha kazi za kisanii na filamu za kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu.
Kipindi cha kujihami kutakatifu yaani vita vya miaka saba zilivyoanzishwa na utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein dhidi ya Iran (1980 - 1988), ni kipindi cha dhahabu cha historia ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo sasa yanaingia katika mwaka wake wa 40 kwa mafanikio makubwa. Vita vya kulazimishwa vya miaka 8 vilikuwa skuli ya upendo na kujiamini, kujitolea, kusimama kidete na ushujaa, na hayo yote yamekusanyika katika matamshi yatakayobakia siku zote ya mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayati Imam Ruhullah Khomeini aliyesema: "Sisi tunaweza."
Kaulimbiu hii ya "sisi tunaweza" ndiyo sifa kuu ya kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu, kwani katika upande mmoja wa vita kulikowepo utawala katili wa Saddam Hussein na waungaji mkono wake ambao walikuwa na silaha za kisasa; na upande mwingine wa vita yaani upande wa kambi ya Uislamu ulikuwa umewekewa vikwazo vya pande zote na kunyimwa hata bidhaa ndogo kabisa na za kawaida. Hali hii isiyo na mlingano inaonesha ukatili wa kupindukia uliotawala vita hivyo. Pamoja na hayo wapiganaji wa Kiislamu walitekeleza vyema wajibu wao kwa kutegemea imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja, moyo wa kujitolea kwa ajili ya Uislamu na roho ya kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na wakafanikiwa kuvuruga mahesabu ya ubeberu wa kimataifa kwa kusimama kidete mbele ya silaha za kisasa kabisa zikiwemo zile za kemikali.
"Moyo wa kupigana jihadi" na "kutoshindwa taifa la Iran" uliotawala nchini kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu sasa umekuwa msingi na nguzo muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu. Nguzo hiyo muhimu imezima na kubatilisha njama na mipango ya kishetani ya maadui wa Uislamu na Iran katika vipindi mbalimbali vya historia ya Mapinduzi ya Kiislamu. Ushindi wa imani na masuala ya kiroho dhidi ya dhulma na ukatili wa kipindi cha vita vya miaka 8 ya kujihami kutakatifu ambapo maadui hawakusita hata kutumia silaha za kemikali dhidi ya raia wasio na hatia, haukuruhusu kutwaliwa hata shibri moja ya ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiisalmu Ayatullah Ali Khamenei anasema kuhusu suala hili kwamba: "Kutokana na utendaji wao, wapiganaji wa kipindi cha kujihami kutakatifu wameonesha picha halisi ya dunia iliyokuwa imejaa ukatili na dhulma na iliyokuwa mbali na imani, masuala ya kiroho na uadilifu ya wakati huo, na picha hii inapaswa kuoneshwa kwa walimwengu."
Athari za kipindi cha kijihami kutakatifu kama filamu na vitabu vya kumbukumbu na kusambaza athari na kazi hizo kwa lugha tofauti za dunia ni sawa na kuarifisha utambulisho wa utamaduni na masuala ya kiroho ya taifa la Iran yanayoonesha kwamba, taifa hilo halikurudi nyuma hata hatua moja katika kipindi kigumu na chenye mashaka mengi. "Kusimama imara" huko na "kujitolea" hakuishii katika kipindi makhsusi na kunaweza kuwa na taathira kubwa sana katika kipindi cha sasa ambapo maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu wamezidisha mashinikizo na uhasama dhidi ya taifa la Iran na Waislamu kwa ujumla. Ni kwa kutilia maanani ukweli huo ndipo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akasisitiza kuwa: "Kama ambavyo hapo mwanzoni mwa Mpinduzi ya Kiislamu na kipindi cha kujihami kutakatifu tuliweza kushinda njama za ubeberu za kutaka kung'oa mche mchanga wa Mapinduzi na kuwalazimisha mabeberu kurudi nyuma, hii leo pia tunaweza kubatilisha na kuzima njama zao kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, kuwa hima kubwa na kusimama imara."