Rais Rouhani: Walimwengu wamebainikiwa na ukweli wa Iran na ubabe wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i48426-rais_rouhani_walimwengu_wamebainikiwa_na_ukweli_wa_iran_na_ubabe_wa_marekani
Rais Hassan Rouhani amesema, misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imebainishwa kwa uwazi kabisa katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kueleza kwamba Marekani haikupata mafanikio yoyote katika kikao hicho.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 27, 2018 12:39 UTC
  • Rais Rouhani: Walimwengu wamebainikiwa na ukweli wa Iran na ubabe wa Marekani

Rais Hassan Rouhani amesema, misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imebainishwa kwa uwazi kabisa katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kueleza kwamba Marekani haikupata mafanikio yoyote katika kikao hicho.

Rais Rouhani ambaye amerejea nchini leo kutoka mjini New York alikokwenda kushiriki kikao cha 73 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amewaeleza waandishi wa habari mara baada ya kuwasili mjini Tehran kwamba, haki na ukweli wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wananchi wa Iran na lugha ya ubabe na utumiaji mabavu wa Marekani vimeshuhudiwa kwa uwazi katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hotuba aliyotoa Rais Donald Trump wa Marekani katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kueleza kwamba, hotuba hiyo iliwachekesha tu viongozi wa mataifa ya dunia.

Dakta Ruohani ameashiria pia kufanyika kikao cha kamati ya pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA pembeni ya kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kubainisha kwamba, katika kikao hicho Iran ilipongezwa kwa kuheshimu na kutekeleza makubaliano hayo.

Rais Hassan Rouhani akihutubia kikao cha 73 cha Baraza Kuu la UN

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, katika kikao hicho nchi zinazounda kundi la 4+1, yaani Ufaransa, Uingereza, China na Russia pamoja na Ujerumani ziliunga mkono kwa dhati makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kutangaza kuwa zimeanzisha njia maalumu zitakayotumia kwa ajili ya mawasiliano ya kibenki na Iran.

Rais Rouhani vilevile amesema, katika vikao alivyofanya na viongozi wa nchi mbalimbali, walizungumzia masuala ya uhusiano wa pande mbili na wa kieneo hususan kadhia ya JCPOA pamoja na uhusiano wa kibiashara baina ya pande mbili na akaongeza kwamba: Katika mazungumzo hayo viongozi wa nchi hizo walisisitiza kuwa hawatotekeleza vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

Tarehe 8 Mei mwaka huu, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kujiondoa nchi hiyo katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kurejesha vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran, hatua ambayo ilikoselewa na kupingwa vikali ndani ya nchi hiyo na katika uga wa kimataifa.../