Rais Rouhani: Marekani ndiyo iliyoshindwa kwa kukiuka makubaliano ya kimataifa
Rais Hassan Rouhani amesema: Kwa mtazamo wa kisheria na kisiasa, Marekani ndiyo iliyoshindwa kwa kukiuka makubaliano ya kimataifa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika hafla ya kuanza mwaka mpya wa masomo kwa vyuo vikuu vya Iran.
Rais Rouhani ameashiria malengo ya waendeshaji Ikulu ya White House dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kueleza kwamba: Marekani, ambayo ghaya na lengo lake kuu ni kuufutia uhalali wa kisiasa Mfumo wa Kiislamu, imeanzisha kwanza vita vya kinafsi na kisha imejiingiza kwenye vita vya kiuchumi dhidi ya Iran.
Dakta Rouhani amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu na wananchi wa Iran watazivuka njama zote za maadui kwa umoja na mshikamano na kuongeza kuwa, rais wa Marekani Donald Trump alifanya kila njia ili kulitumia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kutoa pigo kwa Iran na kupata uungaji mkono kwa siasa zake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, lakini wanachama wengine wote 14 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa waliunga mkono makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, katika historia ya Marekani haijawahi kutokea serikali yenye uadui mkubwa zaidi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kama ilivyo timu iliyoko Ikulu ya White House hivi sasa na akafafanua kwamba rais wa Marekani amejitoa kwenye makubaliano ya kimataifa ya baina ya pande kadhaa (yaani JCPOA) bila ya hoja yoyote kinyume na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Rais Rouhani ameongeza kuwa: Kwa mtazamo wa siasa za nje, bila shaka yoyote Iran ni mshindi katika kadhia hiyo, na hakuna mtu yeyote mwenye shaka juu ya hilo; na kila mtu anajua kwamba bila shaka Marekani ndiyo iliyoshindwa kwa mtazamo wa kisheria na kisiasa kwa kukiuka makubaliano ya kimataifa.../