Rais Rouhani: Maadui hawawezi kustahamili izza na nguvu za Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49979-rais_rouhani_maadui_hawawezi_kustahamili_izza_na_nguvu_za_iran
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema kuwa, maadui wa taifa hili hawana chaguo jingine isipokuwa kusalimu amri na kuheshimu izza, uwezo na umoja wa wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 05, 2018 13:01 UTC
  • Rais Rouhani: Maadui hawawezi kustahamili izza na nguvu za Iran

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema kuwa, maadui wa taifa hili hawana chaguo jingine isipokuwa kusalimu amri na kuheshimu izza, uwezo na umoja wa wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu.

Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo mkoani Semnan kaskazini mwa nchi na kuongeza kuwa,  "Maadui wa Iran wameingiwa na kiwewe na kughadhibishwa na uwezo mkubwa wa taifa hili. Hawawezi kamwe kuvumilia nafasi athirifu ya Iran duniani."

Amesema Wairani wanajua na kufahamu vyema maana ya vikwazo, lakini bila shaka watapita kipindi hiki cha changamoto kama walivyofanya huko nyuma.

Rais wa Iran amebainisha kuwa, maadui wa Iran katika nchi za Afghanistan, Iraq, Syria na Lebanon walishindwa kufikia malengo yao ghalati, na katu hawawezi kufanikiwa katika nchi ya Yemen.

Rais Rouhani akihutubia wakazi wa mji wa Shahroud mkoani Semnan

Amesema maadui hawawezi kustahamili Iran imara na yenye nguvu, na taifa la Iran kamwe halijawahi kusalimu amri mbele ya adui na wala halitafanya hivyo.

Rais Hassan Rouhani ameongeza kuwa, njama za maadui wa Iran wanaofanya juu chini kuvuruga usalama na uthabiti katika eneo la Mashariki ya Kati zitagonga mwamba.