Rais Rouhani asisitiza: Iran haitafanya mazungumzo kuhusu uwezo wake wa makombora
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49993-rais_rouhani_asisitiza_iran_haitafanya_mazungumzo_kuhusu_uwezo_wake_wa_makombora
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezihutubu nchi za Ulaya akisema Iran katu haitafanya mazungumzo kuhusu uwezo wake wa kujihami.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 06, 2018 06:39 UTC
  • Rais Rouhani asisitiza: Iran haitafanya mazungumzo kuhusu uwezo wake wa makombora

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezihutubu nchi za Ulaya akisema Iran katu haitafanya mazungumzo kuhusu uwezo wake wa kujihami.

Akizungumza Jumatano ya jana akiwa safarini mkoani Semnan, Hassan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema: "Iwapo nchi za Ulaya zinataka kufanyike mazungumzo kuhusu uwezo wa kujihami wa Iran, hilo ni jambo lisilowezekana kwani uwezo wa kujihami ni kwa ajili ya kuilinda nchi.

Vilevile Mohammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Jumatano pia akizungumza mbele ya waandishi habari alisisitiza kuwa, hakuna nchi inayoweza kuitaka nchi kubwa na inayojitegemea kama Iran isiwe na zana zake za kujihami.

Katika kipindi cha siku za hivi karibuni wakati wa kukaribia mapatano ya Iran na Ulaya kuhusu mfumo wa kifedha wenye lengo la kulinda mapatano ya nyuklia ya JCPOA, watawala wa Marekani wameanzaisha mkakati wa kuvuruga mapatano hayo.

Madai ya Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuwa eti majaribio ya makombora ya Iran yanakiuka azimio 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yametolewa katika hali ambayo, kimsingi azimio hilo halijaizuia Iran kufanya majaribio ya makombora. Kitu ambacho azimio hilo limepinga ni kuunda makombora yenye uwezo wa kusheheni vichwa vya mabomu ya nyuklia. Iran kamwe haina mpango wa kutengeneza zana za nyuklia na makombora yake ni ya kawaida yenye lengo la kujihami na kuimarisha uwezo wa kujilinda mbele ya adui.

Mike Pompeo

Uzushi na madai ya Marekani kuhusu kadhia ya makombora ya Iran ni njia ya kufunika uhalifu na jinsi Marekani yenyewe ilivyokiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama. Marekani, kwa kushirikiana na Ufaransa na Uingereza, zimefeli katika jaribio la kutumia vibaya Baraza la Usalama kufuatilia miradi ya makombora ya Iran. Marekani haiwezi kuficha sera zake za kukiunga maazimio ya Baraza la Usalama kwa kutoa madai yasiyo na msingi. 

Mike  Fitzpatrick Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Kistratijia (IISS) amejibu madai ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na kusisitiza kuwa: "Majaribio ya makombora ya Iran hayakiuki azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Fitzpatric ameongeza kuwa: "Azimio hilo pia linazitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zisichukue hatua ambazo zinaweza kudhoofisha mapatano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA; na Marekani tayari imekiuka takwa hilo."

Marekani daima imekuwa ikifuatilia lengo la kuweka vizingti katika miradi ya kutengeneza makombora ya kujihami ya Iran na serikali ya Rais Donald Trump imetekeleza mikakati kadhaa kwa ajili ya kufikia lengo hilo.

Kujiondoa Marekani katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA kulifanyika kwa lengo hilo hilo na sasa sera hiyo inatekelezwa sambamba na ile ya kueneza chuki dhidi ya Iran kwa kujaribu kuzishwawishi nchi za Ulaya ziiwekee vikwazo Tehran. Mikakati hiyo imepelekea kuitishwe kikao cha Baraza la Usalama lakini Marekani na waitifaki wake kwa mara nyingine wamegonga mwamba.

Katika hali kama hii, nchi za Ulaya hazipaswi kuingia katika mchezo mchafu wa Marekani na sasa zina jukumu la kihistoria la kuokoa mapatano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA.

Kushirikiana nchi za Ulaya  na Marekani kunaonyesha misimamo yao ya kindumakuwili, kwani azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama halijaizuia Iran kufanya jaribio la makombora.

Iran inafuatilia sera za kimantiki kabisa katika mpango wake wa makombora na ni wazi kuwa, nchi ambayo inatekeleza njama za kuweka vizingiti katika kitengo muhimu zaidi cha uwezo wa Iran kuzuia adui yenyewe inatekeleza sera 'mbaya' za 'kuharibu mapatano ya JCPOA machoni mwa nchi za Ulaya'.

Kitu ambacho kinatia wasiwasi ni kuendelea ukosefu wa usalama Asia Magharibi na ni wazi kuwa, makombora ya Iran hayahusiki na hali hiyo kwani hayajawahi kumlenga hata raia moja wa kawaida.

Sera za kindumakuwili za baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani zimechangia kukosekana usalama eneo la Asia Magharibi au Mashariki ya Kati. Hii ni kwa sababu, sambamba na uzushi na madai yanayotolewa kuhusu miradi ya kutengeneza makombora ya kujihami ya Iran, nchi hizo zinatuma idadi kubwa ya silaha kwa baadhi ya tawala za Kiarabu katika eneo hilo jambo ambalo limeendelea kuchochoe ukosefu wa amani Asia Magharibi.