Zanganeh: Kikao cha karibuni cha Opec; pigo jingine kwa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i50137-zanganeh_kikao_cha_karibuni_cha_opec_pigo_jingine_kwa_marekani
Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekitaja kikao kilichofanyika hivi karibuni cha Jumuya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) huko Vienna mji mkuu wa Austria kuwa ni pigo jingine kwa Marekani.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Dec 13, 2018 04:01 UTC
  • Bijan Namdar Zangeneh
    Bijan Namdar Zangeneh

Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekitaja kikao kilichofanyika hivi karibuni cha Jumuya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) huko Vienna mji mkuu wa Austria kuwa ni pigo jingine kwa Marekani.

 Bijan Zanganeh amesema katika mazungumzo maalumu  na kanali ya pili ya televisheni ya Iran kuwa kikao cha hivi karibuni cha jumuiya ya OPEC kilikuwa kigumu na kilifanyika chini ya mashinikizo makali ya Marekani. Ameongeza kuwa nchi mbili jirani ndizo zilizoelekeza mashinikizo mengi kwa Iran katika kikao hicho na hatua ya nchi hizo haikuwa ya kirafiki. 

Waziri wa Mafuta wa Iran aliendelea kubainisha kuwa: Iwapo  Iran ingekubali kupunguza uzalishaji wa mafuta, kiwango cha uzalishaji wake wa bidhaa hiyo kingepungua mapipa laki sita ya mafuta  kwa siku. Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeruhusiwa kuendelea kuzalisha kiwango chake cha sasa cha bidhaa hiyo. 

Zanganeh amesema mwenendo wa sasa wa soko unaonyesha kuwa hatua chanya ya OPEC ya kupunguza uzalishaji mafuta imekubaliwa na kusisitiza kuwa, jumuiya hiyo inakabiliwa na vitisho ambavyo baadhi yake ni kutoka nje na vingine vya ndani. Waziri wa Mafuta wa Iran amesema hakuna tofauti baina ya mafuta ghafi na bidhaa zitokanazo na mafuta katika upande wa vikwazo vya Marekani.

Kikao cha 175 cha Jumuiya ya Opec kilifanyika tarehe 6 na 7 mwezi huu wa Disemba mjini Vienna Asutria. 

Washiriki wa kikao cha Opec katika mahojiano na waandishi wa habari  
 

Katika kikao hicho, nchi wanachama zimekubaliana kupunguza uzalishaji wa mafuta wa mapipa laki nane kwa siku lakini Iran,Venezuela na Libya hazikujumuisha kwenye makubaliano hayo ya kupunguza uzalishaji wa bidhaa hiyo.