Admeri Shamkhani: Hakuna nchi yenye uthubutu wa kuishambulia kijeshi Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i50714-admeri_shamkhani_hakuna_nchi_yenye_uthubutu_wa_kuishambulia_kijeshi_iran
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia uwezo wa kiulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema kuwa, taifa hili lina nguvu na uwezo kiasi kwamba, hakuna nchi inayoweza kuthubutu kuishambulia kijeshi.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 07, 2019 23:03 UTC
  • Admeri Ali Shamkhani
    Admeri Ali Shamkhani

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia uwezo wa kiulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu na kusema kuwa, taifa hili lina nguvu na uwezo kiasi kwamba, hakuna nchi inayoweza kuthubutu kuishambulia kijeshi.

Admeri Ali Shamkhani alisema hayo jana Jumatatu katika "Kongamano la Kimataifa la Kiulinzi na Kiusalama Katika Magharibi mwa Asia" na kubainisha kwamba, Iran haina vikosi katika eneo fulani hata itake kuviondoa.

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, wananchi wa Iraq, Syria, Afghanistan na Yemen wao wenyewe wana uwezo wa kulinda nchi zao.

Admeri Shamkhani ameongeza kuwa, Iran imetuma kwa matakwa ya nchi husika washauri wa kijeshi katika nchi kama Syria na nyinginezo na kwamba, hilo limetimia kwa ridhaa kamili ya serikali husika.

Brigedia Jenerali Amir Hatami, Waziri wa Ulinzi wa Iran akitazama kombora la "Fat'hul Mubin", moja ya makombora ya kisasa ya Iran

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia suala la kufanyika mazungumzo ya Marekani na Iran na kusema kuwa, Wamarekani wameshathibitisha kwamba, hawana muamana na si watu wa kuaminika hata kidogo na hilo linaungwa mkono na historia ya mazungumzo.

Aidha kuhusiana na mazungumzo ya Iran, kundi la wanamgambo wa Taliban na serikali ya Afghanistan, Admeri Ali Shamkhani amesema kuwa, Tehran inataka kuisaidia serikali ya Kabul ili iweze kufikia ufumbuzi kuhusiana na matatizo inayokabiliwa nayo na hivyo kurejesha amani na utulivu katika nchi hiyo.