Kharrazi: Kitendo cha nchi za Ulaya cha kuchelewesha utekelezaji wa SPV hakikubaliki
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i50984-kharrazi_kitendo_cha_nchi_za_ulaya_cha_kuchelewesha_utekelezaji_wa_spv_hakikubaliki
Mkuu wa Baraza la Kiistratijia la Uhusiano wa Kigeni la Iran amezilaumu nchi za Ulaya kwa kuchelewa kutekeleza mfumo maalumu wa kubadilishana fedha na Iran maarufu kwa jina la SPV na kusema kuwa, kisingizio kinachotolewa na nchi hizo cha kwamba haziwezi kuyalazimisha mashirika ya nchi zao, hakikubaliki kabisa.
(last modified 2025-10-19T03:07:26+00:00 )
Jan 19, 2019 16:37 UTC
  • Kharrazi: Kitendo cha nchi za Ulaya cha kuchelewesha utekelezaji wa SPV hakikubaliki

Mkuu wa Baraza la Kiistratijia la Uhusiano wa Kigeni la Iran amezilaumu nchi za Ulaya kwa kuchelewa kutekeleza mfumo maalumu wa kubadilishana fedha na Iran maarufu kwa jina la SPV na kusema kuwa, kisingizio kinachotolewa na nchi hizo cha kwamba haziwezi kuyalazimisha mashirika ya nchi zao, hakikubaliki kabisa.

Kamal Kharrazi ambaye pia ni waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Iran amesema hayo wakati alipoonana na ujumbe kutoka Italia hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, kama nchi za Ulaya zilikuwa zinatambua kwamba haziwezi kuyashinikiza mashirika yao, kwa nini ziliamua kufanya mazungumzo na Iran?

Ujumbe wa Iran ukiongozwa na Kamal Kharrazi katika mazungumzo na ujumbe wa Italia mjini Tehran

 

Vile vile amesema, kinachotafutwa na rais wa Marekani, Donald Trump, ni kuligawa vipande vipande bara Ulaya na kwamba kitendo cha Marekani cha kuitisha kikao kilicho dhidi ya Iran huko Poland ni sehemu ya njama za Trump za kuzusha mizozo kati ya nchi za Ulaya.

Aidha amesema, Iran imeonesha kivitendo nia yake njema kuhusu mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Ameongeza kuwa, walio wengi nchini Iran wana wasiwasi tangu zamani kuhusu nia ya nchi za Ulaya ya kuheshimu mapatano ya JCPOA na hivi sasa ni kwa faida ya Ulaya kuchukua hatua za kivitendo za kuimarisha mapatano hayo. 

Pande zilizobakia katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA

Mkuu huyo wa Baraza la Kiistratijia la Uhusiano wa Kigeni la Iran pia amesema, kusalimu amri nchi za Ulaya mbele ya mashinikizo ya Marekani hasa hivi sasa kutaifanya Washington izishinikize zaidi nchi hiyo na kuvunjika mapatano ya JCPOA nako bila ya shaka kutakuwa na madhara kwa nchi za Ulaya yakiwemo ya kiusalama.