Jeshi la Iran lamaliza mazoezi kwa mafanikio
Jeshi la Nchi Kavu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo limemaliza mazoezi makubwa ya kijeshi yaliyopewa jina la "Iqtidar 97" ambayo yalianza Ijumaa katika eneo la Isfahan.
Msemaji wa mazoezi hayo, Brigedia Jenerali Nozar Neemati amesema mazoezi hayo yamefanyika kwa mafanikio na kufikia malengo yote yaliyoainishwa.
Amesema katika siku ya mwisho ya mazoezi hayo, Jeshi la Nchi Kavu la Iran, limefanya mazoezi ya ufyatuaji mizingia na radiamali ya haraka yenye lengo la kuhujumu. Aidha amesema katika mazoezi hayo, wanajeshi wamefanya oparesheni za kumfuatilia na kumaungamiza kikamlifu adui kwa mafanikio.
Brigedia Jenerali Neemati ameongeza kuwa, katika mazoezi hayo majeshi ya Iran yameweza kuonyesha uwezo wa kutekeleza oparesheni kwa kasi kubwa.
Aidha amesema kwa mara ya kwanza katika mazoezi hayo, majeshi ya Iran yametekeleza mradi wa 'kilomita sita za ukuta wa moto' ambapo adui hakuweza kupenye katika ukuta huo.'
Wakati huo huo Mkuu wa Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Mohammad Baqeri amesema, Iran italazimika kutumia mbinu za kushambulia ili kulinda maslahi yake na wakati huo huo itaendelea na sera zake jumla za kujihami.
Amesema Iran haina lengo la kuvamia na kukalia kwa mabavu ardhi ya nchi yoyote wala haina lengo la kudhuru maslahi ya wengine bali kile ambacho inafuatilia ni kulinda mafanikio na maslahi ya kitaifa na inaweza kufuatilia sera za kushambulia katika suala hilo.
Brigedia Jenerali Baqeri amesema iwapo yeyeto atalenga kuihujumu Iran au iwapo kutakuwa na ishara za hilo, basi Jamhuri ya Kiislamu itashambulia na haitakaa na kusubiri kuona utulivu wa nchi unavurugwa.