Rouhani: Mapinduzi ya Kiislamu yaliyashinda madola ya kibeberu kwa kusimama kidete wananchi
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa hayati Imam Ruhullah Khomeini ni mhuishaji mkubwa zaidi wa dini katika zama za sasa na ndiye mhandisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ambayo yalipata ushindi dhidi ya madola ya kibeberu kutokana na kusimama kidete kwa wananchi.
Rais Rouhani ameyasema hayo leo katika sherehe iliyofanyika kutangaza tena utiifu wa baraza la mawaziri kwa malengo ya mwasisi wa Jamhurii ya Kiislamu, Imam Khomeini na katika mlolongo wa maadhimisho ya mwaka wa 40 wa Mapinduzi ya Kiislamu. Amelipongeza taifa la Iran kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kusema: Kilichotokea miaka arubaini iliyopita hapa nchini ni tukio la aina yake katika historia.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema kuwa Imam Khomeini aliwatia matumaini wananchi kuhusu mustakbali bora zaidi, nchi huru na inayojitawala, inayotawaliwa na wananchi kwa mujibu wa sheria za Kiislamu, na matumaini hayo yaliwahamasisha zaidi wananchi.
Amesema kuwa kazi kubwa ya hayati Imam Ruhullah Khomeini ni kuasisi utawala wa Kiislamu na kuongeza kuwa, muda mfupi baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuliundwa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu na katiba mpya ikaandikwa na kupigiwa kura ya maoni ya wananchi.
Rais Rouhani pia ameashiria mazungumzo ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 na kusema kuwa: Mazungumzo hayo ya Iran na madola 6 makubwa duniani ni miongoni mwa fahari kubwa za kisiasa za Iran katika miongo na karne kadhaa za hivi karibuni, na ushindi ilioupata Iran katika nyanja mbalimbali kwenye mazungumzo hayo kaumwe hautatoweka.
Amesisitiza kuwa, wakati wa sasa ni wakati wa umoja na mshikamano na kwamba Imam Khomeini alisisitiza zaidi juu ya udharura wa kulindwa umoja hapa nchini.