Rais Rouhani: Wananchi wa Venezuela watasambaratisha njama mpya za Marekani
(last modified Sat, 02 Feb 2019 14:43:18 GMT )
Feb 02, 2019 14:43 UTC
  • Rais Rouhani: Wananchi wa Venezuela watasambaratisha njama mpya za Marekani

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, wananchi wa Venezuela watasambaratisha njama mpya za Marekani kwa kudumisha umoja na kusimama kidete pamoja na serikali.

Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo wakati alipokuwa akipokea hati ya utambulisho ya Carlos Antonio Alcalaa, balozi mpya wa Venezuela hapa mjini Tehran ambapo sambamba na kubainisha kuwa, Marekani imeanzisha njama mpya dhidi ya serikali na taifa la Venezuela, ameeleza kuwa, kimsingi serikali ya Washington inapinga mapinduzi yote ya wananchi na madola huru na inataka kudhibiti ulimwengu kupitia kukandamiza mapinduzi na madola huru na yasiyokubali kunyongeshwa.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza tena himaya na uungaji mkono wa Tehran kwa serikali halali ya Rais Nicolas Maduro wa Venezuela na kusema kuwa, umoja wa wananchi wa nchi hiyo na serikali halali ni muhimu mno na kwamba, hatua hiyo itasambaratisha njama mpya dhidi ya taifa la Venezuela.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

Rais Rouhani ameashiria uhusiano mzuri uliopo baina ya Tehran na Caracas na kusema kuwa, Iran itaendelea kustawisha uhusiano wake na Venezuela katika nyanja za siasa, uchumi na uwekezaji vitega uchumi.

Kwa upande wake Carlos Antonio Alcalaa, balozi mpya wa Venezuela hapa mjini Tehran amesifu na kuthamini uungaji mkono wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, serikali na wananchi wa Iran kwa wananchi na serikali ya Venezuela katika vipindi tofauti na kusema kuwa, wananchi wa nchi yake watapata ushindi katika vita hivi vipya.

Tags