Russia: Mpango wa makombora wa Iran haukiuki sheria za kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51495-russia_mpango_wa_makombora_wa_iran_haukiuki_sheria_za_kimataifa
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza kuwa Iran ina haki ya kujilinda, na mpango wake wa makombora haukiuki sheria za kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 12, 2019 00:59 UTC
  • Russia: Mpango wa makombora wa Iran haukiuki sheria za kimataifa

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza kuwa Iran ina haki ya kujilinda, na mpango wake wa makombora haukiuki sheria za kimataifa.

Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya al-Mayadeen, Segei Ryabkov ameongeza kuwa, Moscow inafanya juhudi za kuweza kushiriki kikamilifu katika mfumo wa mabadilishano ya kifedha kati ya Ulaya na Iran unaojulikana kama Instex.

Katika miezi ya karibuni, serikali ya Marekani imedai mara kadhaa kwamba, shughuli za anga za mbali na za makombora ya Iran zinakiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, madai hayo ya viongozi wa Marekani ni "uongo mkubwa" na akabainisha kwamba, kutokana na hatua ya pupa na isiyo ya kimantiki iliyochukua ya kujitoa kwenye makubaliano ya JCPOA, ambayo ni maelewano maalumu ya kimataifa, na kufuatia kutengwa kimataifa kwa hatua yake hiyo, Marekani inajaribu kwa kila namna kuzusha masuala ya aina hiyo ili kufunika makosa ya kistratejia iliyofanya kuhusiana na JCPOA.

Ofisi ya Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya nayo pia imetangaza kuwa, majaribio ya makombora yanayofanywa na Iran hayakiuki makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.../