Iran na Uganda zasisitiza kustawisha uhusiano wao wa pande mbili
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Uganda na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo wamesisitiza kustawishwa uhusiano wa pande mbili katika nyanja mbali mbali.
Katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Sam Kutesa yaliyofanyika mjini Kampala, Sayyed Morteza Mortazavi, balozi wa Iran nchini humo ameashiria hali ilivyo hivi sasa katika uhusiano wa pande mbili, matukio ya kieneo na kimataifa pamoja na kutatuliwa vizuizi vilivyopo na akataka zifanyike juhudi zaidi kwa ajili ya kutekelezwa hati za maelewano zilizosainiwa na nchi mbili.
Mortazavi aidha amemkabidhi Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda barua ya mwaliko wa kuitembelea Tehran kutoka kwa waziri mwenzake wa Iran Mohammad Javad Zarif.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda amekaribisha ushiriki wa mashirika ya Iran katika utekelezaji wa miradi na mipango ya ustawi wa kiuchumi nchini Uganda.
Kutesa ameongeza kuwa: Uganda inafanya juhudi za kuandaa mazingira yanayohitajika kwa ajili ya kuvutia uwekezaji na ushirikiano na mashirika ya kigeni, ambapo katika hilo inayaalika mashirika ya Iran yenye hamu ya kwenda kuwekeza mitaji na vitega uchumi nchini humo.
Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda amebainisha pia kuwa ,mielekeo ya baadhi ya nchi ya kuchukua maamuzi ya upande mmoja haikubaliki, na akafafanua kwamba: Uganda ni nchi inayojitawala na wala hailazimiki kufuata maamuzi ya nchi zingine yanayolenga kutoa mashinikizo kwa kutoshirikiana na nchi fulani.../