Umoja wa Mataifa: Iran inaongoza kuhusu kuheshimu haki za binaadamu magharibi mwa Asia
Naibu Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Iran ni moja ya nchi zinazoongoza kuhusiana na suala la kuheshimiwa haki za binaadamu katika eneo la magharibi mwa Asia na kuongeza kuwa, wanawake wa Iran wako katika mstari wa mbele katika nyanja tofauti.
Kate Gilmore ameyasema hayo alipokutana na Farideh Oladghobad, Mkuu wa Mrengo wa Wanawake katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran, (yaani bunge) pamoja na wajumbe wengine wa mrengo huo mjini Tehran ambapo sambamba na kubainisha kwamba masuala ya haki za binaadamu hayatakiwi kuwa ya kisiasa, ameongeza kwamba Umoja wa Mataifa umekinai kuhusiana na hali ya haki za binaadamu nchini Iran. Kadhalika Gilmore amelaani vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu, ubaguzi uliojengeka juu ya misingi ya rangi na hatua za upande mmoja. Kwa upande wake Bi Farideh Oladghobad amesisitizia umuhimu wa suala la haki za binaadamu duniani na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina mtazamo wa kipekee kuwahusu wanawake na kulindwa utukufu wa kibinaadamu wa wanawake.
Aidha Oladghobad ameashiria propaganda za vyombo vya habari vya kigeni kuhusiana na wanawake na watu wa jamii za wachache za kidini nchini Iran na kusema, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wanawake nchini hapa wamepata nafasi athirifu katika nyuga tofauti za kisiasa, kiuchumi, kielimu na kijamii. Mkuu wa Mrengo wa Wanawake katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran, pia amegusia suala la migogoro ya Yemen na Myanmar na kubainisha kwamba, wanawake na watoto ni wahanga wakubwa wa vita na mauaji katika nchi hizo, hivyo kuna udharura wa kufuatiliwa suala hilo haraka.