Jan 23, 2026 03:20 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Ijumaa tarehe Tatu Rajab 1447 Hijria sawa na 23 Januari mwaka 2026.

Siku kama ya leo miaka 1443 iliyopita, alizaliwa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (saw).

Kipindi bora cha maisha ya Imam Hussein (as) ni cha miaka sita wakati mtukufu huyo alipokuwa pamoja na babu yake, Mtume (saw). Imam Hussein (as) alijifunza maadili mema na maarifa juu ya kumjua Mwenyezi Mungu kutoka kwa baba yake Imam Ali (as) na mama yake Bi Fatimatul-Zahra (as), ambao walilelewa na Mtume Mtukufu.

Imam Hussein alishiriki vilivyo katika matukio mbalimbali wakati Uislamu ulipokabiliwa na hatari. Daima alilinda turathi za thamani kubwa za Mtume kwa kutoa darsa na mafunzo kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya kiitikadi, kifikra na kisiasa. Imam Hussein (as) alichukua jukumu la kuuongoza umma wa Kiislamu mwaka 50 Hijria, baada ya kuuawa shahidi kaka yake Imam Hassan (as). Hatimaye Imam Hussein (as) aliuawa shahidi huko Karbala mwaka 61 Hijria wakati akitetea dini tukufu ya Kiislamu. 

Katika siku kama ya leo miaka 1387 iliyopita, msafara wa Imam Hussein (as) mjukuu wa Bwana Mtume (saw) uliwasili katika mji wa Makka.

Imam Hussein ambaye alikuwa amehatarisha maisha yake kwa kuupinga utawala wa Yazid na kukataa kumpa baina na mkono wa utiifu kiongozi huyo, aliondoka Madina na kuelekea Makka.

Alipowasili mjini Makka Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib alilakiwa na watu wengi na shakhsia wakubwa wa mji huo na akaamua kuitumia fursa ya uwepo wa Mahujaji kwa ajili ya kufichua ufisadi wa Bani Ummayah hususan Yazid bin Muawiya na kwa muktadha huo akawa amefikisha ujumbe wake katika pembe mbalimbali za maeneo ya Waislamu. Aidha akiwa mjini Makka Imam Hussein alipokea maelfu ya barua kutoka kwa wakazi wa mji wa Kufa Iraq ambao mbali na kutangaza kuupinga utawala wa Yazid walimtaka Imam aelekee katika mji huo.

Baada ya kukaa kwa takribani miezi mine mjini Makka na kwa kuzingatia mwaliko wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na kutokana na hatari iliyokuwa ikimkabili kutoka kwa makachero wa Yazid, tarehe 8 Dhulhija mwaka 60 Hijria, alielekea katika mji wa Kufa.   

Miaka 194 iliyopita katika siku kama ya leo Edouard Manet mchoraji mahiri wa Kifaransa alizaliwa. Awali Edouard alikuwa na mapenzi makubwa na ubaharia.

Hata hivyo baadaye alianza kujihusisha na uchoraji na kuonyesha kipaji kikubwa katika sanaa hiyo. Kazi zake ziliwavutia wengi. Edouard Manet aliaga dunia 1883.

Siku kama ya leo miaka 128 iliyopita alizaliwa Ayatullah Hussein Khadimi, faqihi, alimu na mujtahidi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu.

Baada ya kuhitimu masomo ya msingi na ya kati alielekea Najaf, Iraq na kupata elimu kwa maulama wakubwa wa zama. Alifikia daraja ya ijtihadi akiwa na umri wa miaka 26 na baada ya kurejea Isfahani alijikita katika shughuli ya kufundisha sheria za Kiislamu (fiqhi) na usulu fiqhi.

Katika tukio la amri ya mtawala wa wakati huo wa Iran ya kuwataka wanawake wavue vazi la staha la hijabu, Ayatullah Hussein Khadimi alitoa hotuba kali ya kupambana na utawala wa Reza Shah Pahlavi kama ambavyo pia alishiriki katika harakati mbalimbali za kupambana na njama za mkoloni Mwingereza kwa ajili ya kupora raslimali za Iran.   

Katika siku kama ya leo miaka 128 iliyopita alizaliwa Sergei Mikhailovich Eisenstein mwananadharia na muongozaji wa filamu wa nchini Russia. 

Aliongoza na kutengeneza filamu yake ya kwanza mwaka 1925 iliyojulikana kwa jina la Strike yaani mgomo. Filamu ya pili ya Sergei Mikhailovich Eisenstein iliyojulikana kwa jina la Battleship Potemkin ilileta mageuzi makubwa katika Sanaa ya filamu na sinema ulimwenguni.

Miongoni mwa athari nyingine za Mikhailovich ni Seed of Freedom, Ten Days that Shook the World na Time in the sun. Mwongozaji filamu huyo aliaga dunia 1948.

Katika siku kama ya leo miaka 107 iliyopita yaani tarehe 23 Januari 1919, Chama cha Kifashisti cha Italia kiliasisiwa na Benito Mussolini. Wanachama wa chama hicho walikuwa wakivaa mashati meusi kama sare zao.

Sare hiyo ilipelekea wafuasi wa chama hicho kujulikana kwa jina la watu wa " Mashati Meusi'.'' Fikra za Kifashisti zilikuwa zimejengeka juu ya misingi ya kuunda dola moja kubwa la kidikteta na fikra hizo zilikuwa zikipingana na aina yoyote ya uhuru. Oktoba mwaka 1922, Benito Mussolini na wafuasi wake waliuteka mji wa Roma na yeye mwenyewe akashika hatamu za uongozi akiwa Waziri Mkuu. Kuanzia hapo kiongozi huyo alianza kutekeleza malengo na sera za Chama cha Kifashisti.

Hata hivyo mwaka 1945, mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia Benito Mussolini alitiwa mbaroni na wazalendo na kisha akanyongwa.   

Miaka 76 iliyopita katika siku kama ya leo, Bunge la utawala haramu wa Israel (Knesset) liliutangaza mji wa Baitul Muqaddas ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu, kuwa mji mkuu wa utawala huo badala ya Tel Aviv.

Uamuzi huo uliofikiwa na Bunge hilo miaka miwili tu baada ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi za Wapalestina, uliwakasirisha mno Waarabu na Waislamu.

Njama hiyo ya Israel iliyolenga kupata ridhaa ya nchi nyingine ili ziutambue rasmi mji huo kama mji mkuu wake na hivyo zihamishie balozi zao katika mji huo, haikuwa na natija, kwani hadi leo mji wa Tel Aviv ungali unatambuliwa kama mji mkuu wa utawala huo vamizi unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina. 

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Bahman 1357 Hijria Shamsia, baada ya kupatikana uhakika kuhusiana na uamuzi wa Imam Khomeini wa kurejea Iran akitokea uhamishoni Ufaransa, kuliundwa kamati ya mapokezi ya Imam Khomeini. Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 50,000 ikiwa na mjumuisho mkubwa wa wawakilishi kutoka vyama na makundi mbalimbali ya mapinduzi. Jukumu kuu la kamati hiyo lilikuwa ni kumpokea Imam Khomeini, kumlinda, kuweka nidhamu, kulinda usalama na kudhamini mambo ya lazima kwa ajili ya kurejea Imam Khomeini.