Ramaphosa atangaza hatua mpya kukabili uhamiaji haramu Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138978-ramaphosa_atangaza_hatua_mpya_kukabili_uhamiaji_haramu_afrika_kusini
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ametangaza msururu wa hatua mpya zinazolenga kukabiliana na uhamiaji haramu, kufuatia kuongezeka kwa wasiwasi wa umma kuhusu suala hilo.
(last modified 2026-06-08T11:12:01+00:00 )
Jun 08, 2026 11:10 UTC
  • Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa
    Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ametangaza msururu wa hatua mpya zinazolenga kukabiliana na uhamiaji haramu, kufuatia kuongezeka kwa wasiwasi wa umma kuhusu suala hilo.

Katika hotuba ya kitaifa Jumapili usiku mjini Pretoria, mji mkuu wa kiutawala, Rais alisema Baraza la Mawaziri limepitisha Mkakati Jumuishi wa Usimamizi wa Uhamiaji, unaolenga kuimarisha utekelezaji wa sheria za uhamiaji, kulinda mipaka, kupambana na rushwa, pamoja na kuboresha mfumo na sera za uhamiaji.

Chini ya mkakati huo mpya, Ramaphosa alisema serikali itaongeza juhudi za kuwabaini na kuwarejesha makwao wahamiaji wasio na vibali halali, kuanzisha mahakama maalum za uhamiaji ili kuharakisha mchakato wa kufukuzwa walioingia nchini humo kinyume cha sheria, kuimarisha usalama wa mipaka, na kuweka adhabu kali kwa waajiri wanaowaajiri kwa makusudi raia wa kigeni wasio na nyaraka sahihi.

Hatua hizo zinakuja wakati mjadala kuhusu uhamiaji haramu umejitokeza kwa nguvu katika mijadala ya umma katika miezi ya karibuni, huku baadhi ya makundi ya kijamii yakiandaa maandamano katika miji kadhaa, ikiwemo Johannesburg, Durban, Pretoria na Cape Town.

Ramaphosa amesema Waafrika Kusini wengi wameeleza wasiwasi wao kuhusu shinikizo kwa huduma za umma, ukosefu wa ajira, uhalifu, na ushindani wa fursa za kiuchumi.

Hata hivyo, Rais alionya dhidi ya kuwalaumu wahamiaji kwa changamoto zote za kijamii na kiuchumi zinazolikabili taifa hilo. “Uhamiaji haramu si chanzo cha changamoto zetu zote za kiuchumi,” alisema, akiongeza kuwa ukuaji wa haraka wa uchumi, uwekezaji na uundaji wa ajira ni mambo muhimu katika kushughulikia matatizo mapana ya nchi.

Pamoja na hayo, Ramaphosa alitahadharisha kwamba uhamiaji usio rasmi unaweza kuleta changamoto za kiusalama na kiutawala iwapo hautadhibitiwa, akibainisha kuwa njia za uhamiaji haramu mara nyingi zinaingiliana na shughuli za uhalifu uliopangwa, ikiwemo usafirishaji haramu wa binadamu, unyang’anyi, uchimbaji haramu wa madini, biashara ya dawa za kulevya na utakatishaji fedha.

Aidha, amesisitiza kuwa utekelezaji wa sheria za uhamiaji ni jukumu la dola, na akawaonya raia dhidi ya kujichukulia sheria mkononi.

Ramaphosa amewahimiza Waafrika Kusini kukabiliana na changamoto hiyo kwa umoja, azma na kuheshimu utawala wa sheria, akisisitiza kuwa Afrika Kusini itaendelea kuzingatia maadili ya kikatiba na wajibu wake wa kimataifa, huku ikihakikisha kuwa kila anayeishi na kufanya kazi nchini humo anafanya hivyo kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa Takwimu Afrika Kusini (Statistics South Africa), nchi hiyo inakadiriwa kuwa na wakazi wapatao milioni 3.3 waliozaliwa nje ya nchi, ambapo karibu theluthi mbili wanatoka katika mataifa ya kusini mwa Afrika.