Brigedia Jenerali Momeni: Iran imekamata tani 806 za mihadarati mwaka 2018
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Mihadarati nchini Iran amesema kuwa, mwaka 2018 Tehran ilikamata tani 806 za madawa ya kulevya.
Brigedia Jenerali Eskandar Momeni, amesema hayo mbele ya wajumbe wa Taasisi ya Elimu ya Mashariki na Baraza la Masuala ya Kimataifa la Russia mjini Moscow na kuongeza kuwa, ripoti ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na madawa ya kulevya na uhalifu wa kitaasisi (UNODC) inaonesha kwamba Iran pekee yake imekamata asilimia 76 ya madawa ya kulevya aina ya tiryak, asilimia 67 ya madawa ya kulevya aina ya morphine, na asilimia 17 ya madawa yote ya kulevya aina ya heroine yaliyokamatwa duniani.
Brigedia Jenerali Momeni ameongeza kuwa, kila mwaka Iran inatumia karibu dola bilioni moja kwa ajili ya kuimarisha ulinzi kwenye mipaka yake na kukabiliana na mihadarati na hadi hivi sasa maafisa wa polisi na wa jeshi la Iran elfu tatu na 811 wameshauawa shahidi katika kupambana na magenge ya magendo ya madawa ya kulevya katika kipindi cha miaka 40 iliyopita.
Ameongeza kuwa, juhudi hizo za Iran zimeyalazimisha magenge ya madawa ya kulevya yabadilishe njia zao za kusafirishia kimagendo madawa yao na sasa yanatumia zaidi njia za baharini badala ya nchi kavu.
Itakumbukwa kuwa mkutano huo wa mjini Moscow umetoa fursa kwa nchi mbili za Iran na Russia kutiliana saini makubaliano maalumu ya kushirikiana katika vita dhidi ya madawa ya kulevya.