May 05, 2019 14:27 UTC
  • Zarif: Vikwazo vya Marekani havina athari za kisiasa kwa Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema vikwazo vya Marekani havina taathira yoyote ya kisiasa kwa Jamhuri ya Kiislamu.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika mahojiano na televisheni ya al-Jazeera ya Qatar na kubainisha kuwa, vikwazo hivyo vya upande mmoja vya Marekani sio tu havina athari za kisheria, bali pia havitaathiri kwa njia yoyote ile siasa za Iran kama Washington ilivyotaraji.

Dakta Zarif amefafanua kwa kusema, "Watawala wa Marekani wanataka kulishinikiza taifa la Iran ili libadilishe sera zake. Hivyo ndivyo Marekani imekuwa ikifanya katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, na hususan tangu (Rais Donald) Trump aingie madarakani. Hata hivyo mashinikizo na vikwazo hivyo havitakuwa na taathira zozote za kisiasa." 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza bayana kuwa, Iran na nchi waitifaki wake zimekuwa na mikakati ya kujikinga kutokana na athari za vikwazo, ikiwemo kuisusia sarafu ya dola ya Marekani katika mabadilishano yake ya kifedha sambamba na kubuni mfumo maalumu wa kufanikisha mabadilishano hayo na rafiki zake.

Iran: Tutaendelea kuuza mafuta yetu licha ya vikwazo

Mohammad Javad Zarif amesisitiza kuwa, "Hatua ya Trump ya kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambayo yaliidhinishwa na mtangulizi wake Barack Obama, ni ukiukaji wa sheria na mapatano ya kimataifa. Katika masuala ya uhusiano wa kimataifa, serikali iliyopo mamlakani huwa inatazamwa kama muendelezo wa serikali iliyotangulia."

Kadhalika Dakta Zarif ameimbia kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar kuwa, hatua zote ghalati zinazochukuliwa na Marekani ni kwa ajili ya kutumikia maslahi ya utawala haramu wa Israel.

 

Tags