Iran yalaani jinai za Wazayuni huko Ghaza, Marekani yapongeza jinai hizo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i53296-iran_yalaani_jinai_za_wazayuni_huko_ghaza_marekani_yapongeza_jinai_hizo
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina waliozingirwa kila upande katika Ukanda wa Ghaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 05, 2019 22:38 UTC
  • Iran yalaani jinai za Wazayuni huko Ghaza, Marekani yapongeza jinai hizo

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina waliozingirwa kila upande katika Ukanda wa Ghaza.

Sayyid Abbas Mousavi sambamba na kuwapongeza wanamapambano wa Palestina kwa kutoa majibu makali dhidi ya jinai za Wazayuni amesisitiza kuwa ni haki ya Wapalestina kujihami mbele ya jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni na ameutaka Umoja wa Mataifa na taasisi za kieneo na kimataifa kuchukua hatua za haraka za kuilazimisha Israel ikomeshe jinai zake dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina.

Kombora la wanamapambano wa Palestina

 

Katika upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani jana aliupongeza utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kufanya jinai na kuua watoto wa Kipalestina huko Ghaza. Mike Pompeo ametoa pongezi hizo katika mahojiano aliyofanyiwa na talevisheni ya Fox News ya Marekani na huku akifumbia macho kwa makusudi mashambulizi mengi na jinai za kuchupa mipaka zinazofanywa kila leo na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina hasa wa Ukanda wa Ghaza amedai kuwa eti Israel ina haki ya kujilinda.

Itakumbukwa kuwa tangu Ijumaa usiku hadi hivi sasa ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel zinafanya mashambulizi katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Ghaza uliozingirwa kila upande na Wazayuni hao. Hadi tunaripoti habari hii, Wapalestina 18 walikuwa wameshauawa shahidi na wengine 170 kujeruhiwa katika jinai hiyo mpya ya Wazayuni.

Wanamapambano wa Palestina wamejibu jinai hizo kwa kuvitwanga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa makombora na maroketi zaidi ya 600 na kuwasababishia hasara za roho, mali na saikolojia.