Mazungumzo ya Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na China
Waziri wa Mashauri ya Kiigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye leo aliwasili Beijingi mji mkuu wa China amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Wang Yi.
Katika mazungumzo hayo Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kiigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wang Yi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa China, wawili hao wamejadiliana na kubadilishana mawazo kuhusiana na matukio ya hivi karibuni ya kieneo na kimataifa na uhusiano wa pande mbili.
Aidha mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa China na Iran wamezungumzia njia za kustawishwa zaidi ushirikiano wa Beijing na Tehran kisiasa, kiuchumi na kadhalia.
Mawaziri hao wamejadili pia uamuzi wa hivi karibuni wa Iran wa kusitisha utekelezaji wa baadhi ya ahadi zake kulingana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kufuatia kigugumizi cha madola na kutotekeleza madola hayo ahadi zake.
Safari ya Dakta Zarif mjini Beijing inafanyika wakati huu ambapo vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vinaonekana kupamba moto.
Mapema jana Alhamisi Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran alikutana na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe na mwenyeji wake Taro Kono ambapo walijadili matukio ya hivi karibuni ya JCPOA na hatua za kisheria ambazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua kukabiliana na hatua ya Marekani ya kukiuka mapatano hayo na kuvunja sheria.
Kabla ya hapo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizitembelea India na Turkmenistan baada ya safari ya wiki iliyopita huko Moscow Russia.