May 25, 2019 04:30 UTC
  • Zarif: Iran itashuhudia mwisho wa Trump, na wala si kinyume chake

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itabakia hai kushuhudia hatima ya Rais Donald Trump wa Marekani na wala si kinyume chake.

Muhammad Javad Zarif aliyasema hayo jana alipoulizwa na mwandishi mmoja wa habari kuhusu matamshi ya hivi karibuni yaliyojaa chuki na uhasama ya Trump dhidi ya Wairani, ambapo amesisitiza kuwa kauli hiyo ya rais wa Marekani kwa mara nyingine imeweka wazi namna mwanasiasa huyo analitazama taifa la Iran, licha ya kudai kuwa utawala wake unawajali sana Wairani.

Wiki iliyopita, Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa: Iwapo Iran inataka vita, huo ndio utakuwa rasmi mwisho wa Iran." Aidha siku ya Alkhamisi, Trump alikariri bwabwaja na madai yasio na msingi kuwa Iran ni taifa la kigaidi.

Akijibu matamshi hayo, Zarif amesema, "Iran imekuwepo kwa maelfu ya miaka na itaendelea kusimama imara. Nchi ambayo ndo kwanza imefika katika jumuiya haina haki ya kuzungumza hivyo kuhusu Iran."

Zarif (kulia) na Donald Trump

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa, vita vya kiuchumi vya Trump dhidi ya taifa la Iran ni ugaidi wa wazi. Amesema kitendo cha rais huyo wa Marekani kutaka kuitwisha Iran sera na mitazamo yake ni kisiasa kupitia vikwazo vya kiuchumi, vikiwemo vya chakula na dawa, ndio ugaidi halisi.

Dakta Zarif amesema kwa msingi huo nembo hiyo ya ugaidi inapaswa kuvaliwa na Trump mwenyewe na wala sio taifa la Iran.

Tags