"Iran haihitajii Marekani wala haitaki kuwa na uhusiano nayo"
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu haihitajii Marekani wala haina haja ya kuwa na uhusiano na Washington.
Muhammad Javad Zarif alisema hayo jana mbele ya kikao cha Kamati ya Usalama wa Taifa na Masuala ya Kigeni ya Bunge la Iran na kufafanua kuwa, Marekani inapaswa kukomesha tabia yake ya kuingilia uhusiano wa Tehran na nchi nyingine.
Amesema vita vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Iran vinatazamwa na taifa hili kama ugaidi wa kiuchumi na jambo hilo linapaswa kukomeshwa mara moja.
Dakta Zarif ameeleza bayana kuwa, "Marekani haipaswi kufanya chochote (kwa maslahi ya Iran), inachotakiwa kufanya ni kuacha kuvuruga uhusiano wa taifa hili na mataifa mengine ya dunia."
Ameashiria kuhusu safari tarajiwa ya Shinzo Abe, Waziri Mkuu wa Japan hapa Tehran wiki hii na safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujuerumani, Heiko Maas ambaye aliwasili hapa Tehran jana Jumapili.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza kuwa, mazungumzo kati ya Ujerumani na Iran yatajikita zaidi katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Amebainisha kuwa, kwa mtazamo wake haoni kama mwanadiplomasia huyo wa Ujerumani amekuja na ujumbe wowote mpya kwa Iran katika safari yake hii na kusisitiza kuwa nchi za Magharibi zinapaswa kutekeleza wajibu wao wa kuyanusuru mapatano hayo ya kimataifa.