Sanders: Trump amelazimika kuzima moto aliouwasha dhidi ya Iran
Seneta Bernie Sanders ambaye ametangaza azma yake ya kugombea tena urais katika uchaguzi wa urais nchini Marekani mwaka ujao amesema Rais Donald Trump wa nchi hiyo amelazimika kuzima moto wa mgogoro na taharuki aliouwasha mwenyewe dhidi ya Iran.
Sanders ameyasema hayo katika mahojiano na mtangazaji Margaret Brennan anayeendesha kipindi cha “Face the Nation” katika kanali ya televisheni ya CBS News na kuongeza kuwa, Trump amechangia pakubwa kushadidi mgogoro baina ya Washington na Tehran.
Huku akikejeli hatua ya Trump ya kuagiza shambulizi dhidi ya Iran na kisha kujisifu kwa kulisimamisha, Sanders amesema, "Kitendo hicho cha Trump ni sawa na kuchoma moto karatasi zilizojaa kwenye jaa, kisha ukauzima moto huo mwenyewe. Binafsi alisaidia kuongezeka taharuki kisha akalazimika kusimamisha shambulizi."
Seneta huyo ambaye amekuwa akisosoa vikali sera na misimamo ya Trump amemshangaa rais huyo wa Marekani kwa kudai kuwa kuingia katika vita na Iran kutakuwa kwa maslahi kwa Wamarekani.
Seneta huyo wa Vermont hivi karibuni pia aliionya vikali serikali ya Trump, dhidi ya kutumia tukio la kushambuliwa meli za mafuta katika Bahari ya Oman kama kisingizio cha kuanzisha vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.