Lavrov: Makundi ya kigaidi yanaitambua Iran kuwa ni adui wao mkuu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54413-lavrov_makundi_ya_kigaidi_yanaitambua_iran_kuwa_ni_adui_wao_mkuu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amepinga madai ya Marekani kwamba Iran inaunga mkono ugaidi na kusisitiza kuwa, makundi ya kigaidi yanaitambua Jamhuri ya Kiislamu kuwa ndiye adui wao mkuu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 28, 2019 02:46 UTC
  • Lavrov: Makundi ya kigaidi yanaitambua Iran kuwa ni adui wao mkuu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amepinga madai ya Marekani kwamba Iran inaunga mkono ugaidi na kusisitiza kuwa, makundi ya kigaidi yanaitambua Jamhuri ya Kiislamu kuwa ndiye adui wao mkuu.

Sergey Lavrov amesema Washington inadai kuwa Iran ni muungaji mkono mkuu wa ugaidi duniani ilhali makundi na taasisi nyingi za kigaidi zilizowekwa kwenye orodha ya Marekani ya makundi ya kigaidi yanaitambua Tehran kuwa ndiye adui wao mkuu. 

Maafisa wa serikali ya Marekani akiwemo Rais Donald Trump wamekuwa wakiituhumu Jamhuri ya Kiislamu kuwa inaunga mkono ugaidi. Hii ni licha ya kuwa Iran ni mhimili wa kambi ya muqawama na mapambano na imekuwa na nafasi kubwa katika kukabiliana na njama za Marekani, Israel na Saudi Arabia, ambazo ndio waungaji mkono wakuu na hata waanzilishi wa kundi la kigaidi la Daesh katika nchi za Syria na Iraq.

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh

Iran pia ilikuwa ya kwanza kutuma washauri wa kijeshi kwenda kupambana na makundi ya kigaidi huko Iraq na Syria baada ya kupokea mwaliko rasmi wa serikali za nchi hizo, suala ambalo liliwakasirisha viongozi wa Marekani na washirika wao. 

Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 na kufuatiwa na Iraq mwaka 2014 baada ya makundi ya kigaidi yaliyokuwa yakifadhiliwa na Marekani, Saudi Arabia, Israel na washirika wao kuzivamia nchi hizo kwa shabaha ya kubadili mlingano wa nguvu za kijeshi katika eneo hilo kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel. Hata hivyo njama hiyo imefeli na virango vya makundi ya kigaidi kama Daesh vimekunjwa kabisa katika nchi za Iraq na Syria kwa msaada wa Iran.