Rouhani amwambia Macron: Umoja wa Ulaya utekeleze majukumu yake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54601-rouhani_amwambia_macron_umoja_wa_ulaya_utekeleze_majukumu_yake
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana usiku alifanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron ambapo amezitaka nchi za Ulaya kutekeleza majukumu yao yanayohusiana na makubaliano ya kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 06, 2019 22:31 UTC
  • Rouhani amwambia Macron: Umoja wa Ulaya utekeleze majukumu yake

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana usiku alifanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron ambapo amezitaka nchi za Ulaya kutekeleza majukumu yao yanayohusiana na makubaliano ya kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Katika mazungumzo hayo, Rais Rouhani ameashiria sisitizo la Rais wa Ufaransa la kulindwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusema: Katika kipindi cha miezi 14 iliyopita Iran imefanya jitihada kubwa za kulinda makubaliano hayo katika fremu ya subira ya kistratijia licha ya mashinikizo yote na vikwazo vya Marekani.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amevitaja vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi ya Marekani dhidi ya Iran kuwa ni harakati ya kigaidi na vita vya kiuchumi vya pande zote na amesisitiza kuwa, kuendelea vita hiyo kunaweza kuzua vitisho vingine katika kanda ya Mashariki ya Kati na duniani.

Rais Rouhani amesema kuwa hatua zilizochukuliwa na Iran hivi karibuni kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA zimefanyika kwa mujibu wa fremu ya makubaliano hayo na kwa shabaha ya kuyalinda na ameutaka Umoja wa Ulaya kutekeleza majukumu yake yanayohusiana na makubaliano ya kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa na kufanya juhudi kubwa zaidi za kulinda makubaliano ya JCPOA. Amesisitiza kuwa, kusitishwa vikwazo vyote kunaweza kuwa mwanzo wa harakati ya Iran na wanachama wa kundi la 5+1. 

Rais Rouhani akiwa pamoja na Macron

Kwa upande wake Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema kuwa tangu hapo mwanzoni Umoja wa Ulaya ulipinga vikali hatua ya Marekani ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuongeza kuwa: Umoja huo unataka kulindwa makubaliano hayo na unafanya jitihada za kuhakikisha yanalindwa. 

Rais wa Ufaransa amesema, anakiri kwamba hatua za Ulaya kwa ajili ya kufidia madhara yaliyosababishwa na vikwazo vya Marekani hazikufanikiwa lakini inafanya jitihada za kufidia nakisi hiyo.