Uwezo wa kiulinzi wa Iran sio wa kutiwa dosari
Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, uwezo wa kiulinzi wa taifa hili si jambo la kutiwa dosari.
Meja Jenerali Muhammad Hussein Baqeri ameashiria matukio ya hivi karibuni katika eneo la Mashariki ya Kati na kueleza kwamba, endapo adui ana tamaa na mambo ambayo ni maslahi ya taifa letu au atachukua hatua ndogo tu ya uvamizi, basi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatoa jibu linalofaa tena kwa wakati mwafaka.
Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, hii kwamba, katika siku za hivi karibuni kulitokea matukio na hadi sasa hawajapata jibu, haina maana ya kukaa kimya au kuukubali uvamizi huo, bali kutatolewa jibu kwa maadui kwa wakati mwafaka na itakapolazimu.
Kwa upande wake, Brigedia Jenerali Amir Hatami, Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kwamba, kusimamishwa meli ya mafuta ya Iran kunakinzana wazi na vigezo na sheria za kimataifa. Aidha amebainisha kwamba, daima Iran imekuwa ikiendesha vita vikali vya kukabiliana na maharamia na bila shaka kitendo hicho cha wanamaji wa Uingereza hakitabakia bila majibu.
Kwa upande wa nguvu na uwezo wa kiulinzi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ipo katika kiwango kizuri na cha kumfanya adui asijaribuu kuanzisha hujuma na mashambulio ambapo mbali na uwezo huo, ina nguvu kubwa ya kushambulia pia endapo hilo litalazimu. Ripoti iliyosambazwa na Taasisi ya Brookings ya Marekani inaonyesha kuwa, Iran ina aina 15 ya makombora ya balestiki ambayo yana uwezo wa kwenda umbali wa kilomita 200 hadi 6000.
Dakta Abd al-Rasool Divsalar, mtaalamu wa masuala ya kiistratejia akitoa tathmini kuhusiana na uwezo wa Iran ambao unamfanya adui asithubutu kuanzisha mashambulio amesema kuwa: Kuna ushahidi na nyaraka nyingi zinazoonyesha kwamba, Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon inaamini kuwa, wakati huu sio kipindi mwafaka cha kuanzisha vita na Iran, kwani vita hivyo vitakuwa na gharama kubwa na kusababisha hasara za kiistratejia, vita ambavyo havitaweza kudhamini malengo ya kisiasa.
Kwa mtazamo wa asasi za utafiti wa masuala ya kijeshi ni kuwa, uwezo wa makombora ya ufukweni kwa baharini, uwezo wa operesheni za boti za kasi za Iran ni changamoto kubwa ya kiteknolojia kwa vikosi vyote vamizi. Aidha ripoti ya taasisi ya Marekani inayohusika na masuala ya kikosi cha majini cha nchi hiyo inaonyesha kuwa, uwezo wa ndege zisizo na rubani za Iran ni moja ya changamoto kubwa za jeshi la Washington katika kukabiliana na Iran.
Umuhimu wa uwezo huu umo katika kalibu ya siasa za kiulinzi za Iran kwa ajili ya kuzuia kutokea vita. Vituo vya utafiti wa kiistratejia vinakiri bayana kwamba, katika fremu ya malengo ya kiistratejia, Iran imeongeza uwezo wake wa kiulinzi kwa ajili ya kukabiliana na vitisho. Miongoni mwa mafanikio ya Iran katika uwanja huo tunaweza kuashiria kutengenezwa nyambizi ya kisasa na makombora ya cruise.
Hapana shaka kuwa, uwezo huu ni wenye kuainisha mambo katika mahesabu na uchukuaji hatua yoyote ile kuhusu machaguzi tarajiwa ya kijeshi. Kwa hakika uwezo wa kutoa jibu katika ulinzi athirifu na nguvu ya kutoa pigo kutoka kwa Iran ni mambo ambayo yamekuwa na taathira kwa mahesabu ya adui. Sababu hizo zimepelekea mahesabu ya kiistratejia yaonyeshe kwamba, endapo Marekani ltaanzisha vita dhidi ya Iran basi itapata hasara kubwa ambayo yumkini isiweze kustahamilika.
Tab'an, hakuna wakati ambao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianzisha vita katika eneo la Mashariki ya Kati au nje ya eneo hili. Lakini kama taifa hili litakabiliwa na tishio na shambulio la kijeshi, basi litatoa jibu kali na kuhami usalama wake.