Ayatullah Hamedani awataka wapigania uhuru kumuunga mkono Sheikh Zakzaky
Ayatullah Hossein Noori-Hamedani mmoja wa marajii taqlidi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia amewataka wapigania uhuru na Waislamu wote ulimwenguni kumuunga mkono Sheikkh Ibrahim, Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
Katika ujumbe wake alioutoa jana, Ayatullah Noori-Hamedani ameonyesha wasiwasi wake kuhusiana na hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky anayeshikiliwa korokoroni na kutangaza kuwa, asasi na jumuiya za kimataifa zimepoteza itibari na utambulisho wake kutokana na kunyamazia jinai mbalimbali na kivitendo taasisi hizo zimekuwa hazina maana.
Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Qum hapa Iran amelaani vikali miamala na vitendo vya serikali ya Nigeria dhidi ya Sheikh Zakzaky, na kuwataka viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufanya kila wawezalo ili kuhakikisha mwanaharakati huyo wa Kiislamu anaachiliwa huru.
Sheikh Zakzaky na mkewe walitiwa mbaroni tarehe 13 Disemba 2015 katika Huseiniya ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria huko Zaria kufuatia shambulio la jeshi la nchi hiyo lililoua shahidi mamia ya Waislamu wasio na hatia.
Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa amri ya kuachiliwa huru mara moja mwanachuoni huyo mwezi Disemba 2016 na kuliwajibisha jeshi la nchi hiyo kuilipa familia ya Sheikh Zakzaky fidia ya dola laki moja na 50 elfu.
Hata hivyo jeshi, serikali na vyombo vya dola vya Nigeria vimekataa kabisa kutekeleza amri hiyo ya mahakama na hadi hivi sasa mwanaharakati huyo wa Kiislamu anaendelea kushikiliwa korokoroni kinyume cha sheria.