Uungaji mkono wa Shekhe wa Muqawama kwa diplomasia ya Zarif
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amemtumia ujumbe Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambapo sambamba na kulaani hatua ya Marekani ya kumwekea vikwazo Mohammad Javad Zarif amesisitizia mshikamano wa muqawama kwa mwanadiplomasia huyo.
Katika ujumbe wake huo, Sayyid Hassan Nasrullah amemhutubu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akisema: "Wewe ni sauti wadhiha na ya wazi katika duru zote za kimataifa na msemaji wa haki mbele ya mataghuti wa dunia."
Tarehe 31 ya mwezi uliopita wa Julai, Wizara ya Fedha ya Marekani ililiweka jina la Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwenye orodha yake ya vikwazo. Hatua hiyo iliyochukuliwa na serikali ya rais wa Marekani Donald Trump inadhihirisha taathira za diplomasia inayofuata msingi wa muqawama katika eneo la Magharibi ya Asia, ambapo kama ulivyopatikana ushindi katika medani za mapambano, imepata mafanikio pia katika uga wa diplomasia.
Diplomasia athirifu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliyofanikiwa kuzima siasa haribifu za serikali ya Marekani na waitifaki wake katika eneo la Magharibi ya Asia ikiwemo katika nchi za Lebanon, Syria, Iraq na Yemen ni muendelezo wa ushindi na sauti ya juu ambayo muqawama umekuwa nayo katika mlingano wa nguvu katika eneo hili.
Mashauriano ya mara kwa mara na diplomasia hai na amilifu ya Iran vimeweza kuelekeza mkondo wa migogoro mbali mbali katika eneo la Magharibi ya Asia katika njia ya mazungumzo kwa ajili ya kutatua migogoro hiyo, mfano hai ukiwa ni mgogoro ulioikumba Syria. Jitihada za mtawalia za diplomasia ya Iran katika kuanzisha "Mchakato wa Astana" zimedhihirisha taathira za diplomasia kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Syria bila kujali irada ya Marekani.
Kufanyika karibu duru 15 za mazungumzo kupitia "Mchakato wa Astana" kwa madhumuni ya kutatua mgogoro wa Syria, ni ishara ya kushinda diplomasia yenye ufanisi ya Iran, ambayo kwa ushirikiano chanya wa Russia na Uturuki imeweza kusambaratisha njama ya pamoja ya mhimili wa Waarabu, Wamagharibi na Waebrania nchini Syria.
Diplomasia hiyo inakamilisha matukio na mabadiliko yanayojiri katika medani za vita nchini Syria na katika eneo zima la Magharibi ya Asia, Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz, ambayo kwa wakati mmoja yameusukuma mbele mwenendo wa mlingano wa nguvu za kijeshi na kisiasa kwa manufaa ya nchi za eneo na kuiweka Marekani kwenye kinamasi cha mkwamo.
Kufungamana pamoja diplomasia na nguvu za kimedani chini ya mhimili wa muqawama, kumesambaratisha siasa za kieneo za Marekani na waitifaki wake; na chambilecho Shekhe wa Muqawama, ni ishara ya ushindi wa haki dhidi ya batili.
Nguvu za kijeshi za mhimili wa muqawama zimeonyesha athari zake katika matukio ya medani za mapambano; na mafanikio hayo yameifanya diplomasia na lugha fasaha ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, akiwa msemaji wa haki katika kukabiliana na mataghuti, ikubalike katika jumuiya za kimataifa.
Uwezo wa kufafanua mambo na wa kujenga hoja za kukubalika wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika duru za kimataifa, umezima njama zinazofanywa katika eneo la Magharibi ya Asia, Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz.
Utunishaji misuli wa Iran katika Ghuba ya Uajemi na "Diplomasia ya Zarif" vimeifanya Marekani na tawala vibaraka na tegemezi kwa Washington zifikirie kuanzisha muungano katika eneo hili kwa kisingizio cha kulinda usalama wa vyombo vya baharini, hatua inayodhihirisha uadui na uhasama wao dhidi ya Iran kutokana na taathira yake katika ushindi wa mhimili wa muqawama.
Mabadiliko ya kisiasa na kijeshi yanayojiri katika eneo la Ghuba ya Uajemi, Syria na Yemen yanadhihirisha nafasi kuu ya Iran katika mlingano wa nguvu za kisiasa kupitia diplomasia na pia kwenye uga wa kimedani kupitia mapambano.
Katika mazingira hayo na kama alivyoeleza Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, vikwazo na hatua za kiuhasama na chuki za Marekani dhidi ya nchi kubwa kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haziwezi kufua dafu, sawa kabisa na Washington ilivyoshindwa na muqawama wa Lebanon licha ya vikwazo ilivyouwekea muqawama huo.../