Kamanda Khanzadi awaambia maadui: Ondokeni Ghuba ya Uajemi au mtaondoka kwa madhila
-
Admeri Hossein Khanzadi
Kamanda wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa majeshi ya adui wa Iran yaliyoko katika Ghuba ya Uajemi yanapaswa kuondoka haraka iwezekanavyo katika eneo hilo la sivyo yataondoka kwa madhila.
Admeri Hossein Khanzadi ambaye alikuwa akizungumza katika sherehe ya kuhitimisha Mashindano ya Kimataifa ya Wapigambizi wa Majeshi ya Dunia yaliyofanyika katika kisiwa cha Kish kusini mwa Iran, amesema kuwa majeshi ya Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni wa Israel yanapaswa kutambua kuwa kambi ya Muqawama na mapambano ya Kiislamu baharini imo katika hali ya kuundika na kipindi cha kupora rasilimali za nchi za kanda hii kimeyoyoma na kutoweka.
"Kipindi cha kupora utajiri wa kanda wa Ghuba ya Uajemi kimekiwisha. Waporaji wanapaswa kuondoka katika eneo hili haraka iwezekanavyo, la sivyo wataondoka kwa madhila", amesisitiza Kamanda wa Jeshi la Majini la Iran.
Admeri Khanzadi ameashiria udharura wa kulindwa amani na usalama wa kanda ya Ghuba ya Uajemi na kusema: Amani ya pande zote ya baharini inahitajia urafiki, ushirikiano, umoja na maelewano katika mazingira ya baharini lakini baadhi ya madola ya kibeberu hayaelewi suala hilo.
Mashindano ya 4 ya Kimataifa ya Wapigambizi wa Majeshi ya Dunia yalimazlika jana katika kisiwa cha Kish. Timu ya wapigambizi ya Jeshi la Majini la Iran imeshika nafasi ya tatu baada ya timu za Russia na China.