Zarif: Marekani haina uwezo wa kuvuruga usalama wa Ghuba ya Uajemi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55541-zarif_marekani_haina_uwezo_wa_kuvuruga_usalama_wa_ghuba_ya_uajemi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inafanya juhudi zake zote kulinda usalama wa Ghuba ya Uajemi na kwamba Marekani haina uwezo wa kuvuruga usalama wa eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 22, 2019 22:14 UTC
  • Zarif: Marekani haina uwezo wa kuvuruga usalama wa Ghuba ya Uajemi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inafanya juhudi zake zote kulinda usalama wa Ghuba ya Uajemi na kwamba Marekani haina uwezo wa kuvuruga usalama wa eneo hilo.

Dk Mohammad Javad Zarif alisema hayo jana mjini Oslo, Norway, na kusisitiza katika kikao cha taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kimataifa ya Norway (NUPI) kwamba Iran kamwe haitoanzisha vita lakini itasimama imara kujihami iwapo itachokozwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, vikwazo vya Marekani vinawalenga moja kwa moja wananchi wa Iran na kusisitiza kwamba huo ni ugaidi wa kiuchumi unaofanywa na Marekani dhidi ya wananchi wa Iran. Ameongeza kuwa, mataifa ya dunia hayapaswi kuiruhusu Marekani izifanyie ubeberu nchi za dunia na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haiwezi kusalimu amri mbele ya mashinikizo na vikwazo vya mabeberu.

Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz

 

Vile vile amegusia jinsi Iran ilivyo na mpaka mkubwa wa majiri katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kusisitiza kuwa, usalama wa Lango Bahari la Hormuz hauwezi kupatikana bila ya kuwepo Iran na hakuna nchi yoyote itakayoruhusiwa kuhatarisha usalama wa eneo hilo kama ambavyo pia Iran iko tayari kushirikiana na nchi nyingine kudhamini usalama wa eneo hilo nyeti na muhimu kiistratijia.

Baada ya Norway, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameelekea nchini Ufaransa kwa ziara rasmi ya kikazi.