Iran yatuma salamu za rambirambi Zimbabwe kufuatia kifo cha Robert Mugabe
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55853-iran_yatuma_salamu_za_rambirambi_zimbabwe_kufuatia_kifo_cha_robert_mugabe
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za rambirambi kwa familia, taifa, serikali na wananchi wa Zimbabwe kufuatia kifo cha baba wa taifa hilo Robert Mugabe aliyefariki dunia hapo jana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 07, 2019 03:39 UTC
  • Iran yatuma salamu za rambirambi Zimbabwe kufuatia kifo cha Robert Mugabe

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za rambirambi kwa familia, taifa, serikali na wananchi wa Zimbabwe kufuatia kifo cha baba wa taifa hilo Robert Mugabe aliyefariki dunia hapo jana.

Sayyid Abbas Mousavi ameashiria mchango usio na mithili wa Robert Mugabe akiwa shujaa katika harakati za ukombozi wa Zimbabwe na kuiondoa nchi hiyo katika makucha ya mkoloni na kusema kuwa, hata baada ya uhuru wa Zimbabwe, Mugabe alisimama kidete kutetea mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Mugabe alisimama imara katika kipindi cha uongozi wake kupinga uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na alikuwa na uhusiano wa karibu na wa kirafiki na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Robert Mugabe kabla ya kufariki dunia alipokuwa matibabuni nchini Singapore

Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe aliaga dunia jana huko nchini Singapore alipokuwa akipatiwa matibabu.

Mwezi Novemba mwaka jana Rais Emerson Mnangagwa wa Zimbabwe  alisema kuwa Mugabe hawezi tena kutembea na amelazwa hospitali nchini Singapore hata hivyo bila ya kusema ni matibabu gani alikuwa akipata nchini humo.

Mugabe ambaye aliiongoza Zimbabwe kwa karibu miongo minne tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka Uingereza mwaka 1980 alilazimishwa kujiuzulu mwezi Novemba mwaka juzi baada ya mapinduzi ya jeshi.