Rouhani: Mazungumzo na Marekani chini ya kivuli cha vikwazo, hayana maana
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55955-rouhani_mazungumzo_na_marekani_chini_ya_kivuli_cha_vikwazo_hayana_maana
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo ya simu ya mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron akisisitiza kuwa, Marekani imekacha kutekeleza majukumu yake kwa kujiondoa katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA na kwamba, kwa mujibu wa mtazamo wa Serikali, Bunge na taifa la Iran, kufanya mazungumzo na Marekani chini ya kivuli cha vikwao hakuna maana yoyote.
(last modified 2026-08-17T09:53:57+00:00 )
Sep 12, 2019 02:58 UTC
  • Rais Hassan Rouhani
    Rais Hassan Rouhani

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo ya simu ya mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron akisisitiza kuwa, Marekani imekacha kutekeleza majukumu yake kwa kujiondoa katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA na kwamba, kwa mujibu wa mtazamo wa Serikali, Bunge na taifa la Iran, kufanya mazungumzo na Marekani chini ya kivuli cha vikwao hakuna maana yoyote.

Rais Rouhani amesema katika mazungumzo hayo ya simu kwamba, iwapo mapatano na Ulaya yatakamilika, Iran iko tayari kurejea katika utekelezaji kamili wa makubaliano ya nyuklia na kwamba kikao cha Iran na kundi la 5+1 pia kinawezekana kufanyika pale vikwazo vitakapoondolewa. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu pia amemshukuru Rais wa Ufaransa kutokana na juhudi zake katika uwanja huu. Vilevile ameashiria hatua ya tatu iliyochukuliwa na Tehran ya kupunguza utekelezaji wa majukumu yake katika makubaliano ya nyuiklia ya JCPOA na kusema: Hatua hiyo imechukuliwa chini ya uangalizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, lakini Iran inaweza kurejea katika hali ya hapo awali.

Rais Rouhani amesema suala la kuimarishwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na usalama wa njia kuu za majini duniani hususan katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman ni malengo mawili muhimu sana kwa Iran na kwamba suala hilo lina faida kwa dunia nzima ukiwemo Umoja wa Ulaya na hata Marekani yenyewe. 

Rais Hassan Rouhani na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron

Kwa upande wake Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameeleza hatua na yaliyojadiliwa katika mazungumzo yake na maafisa wa Marekani na kusema, Paris itaendeleza jitihada za kuhakikisha kwamba makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yanatekelezwa na kunapatikana mwafaka. 

Marais wa Iran na Ufaransa wamekubaliana kudumisha mazungumzo na mashauriano baina ya nchi hizo mbili.