Zarif: Iwapo Marekani inataka mazungumzo na Iran lazima itekeleze ahadi zake
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Iran haitaacha mustakabali wa uchumi na wananchi wake utegemee mkutano wa kimaonyesho na Rais Donald Trump wa Marekani. Ameongeza kuwa, kama ambavyo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alivyosema, 'iwapo Mareknai inataka kufanya mazungumzo na Iran, ni lazima kwanza itekeleze ahadi zake na isitishe vikwazo.'
Mohammad Javad Zarif aliyasema hayo Jumamosi alasiri baada ya kumalizika safari yake ya siku 9 katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York na kuongeza kuwa, 'Iran kamwe haijawahi kuwa nchi yenye kuvunja ahadi zake.'
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha amegusia kuhusu uhusiano wa Iran na Saudi Arabia na ubunifu wa 'Amani ya Hormouz' na kusema, ubunifu huu ni fursa nzuri zaidi kwa Saudi Arabia kujiunga na 'Muungano wa Matumaini."
Zarif amesisitiza kuwa, Iran daima imekuwa ikiwatakia mema majirani zake na kuongeza kuwa: "Daima Iran imekuwa ikizitizama nchi jirani kama ndugu kwani zitabakia kuwa majirani hadi mwisho wa historia."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria namna Iran ilivyoisaidia Kuwait wakati ilipovamiwa na dikteta aliyeangushwa wa Iraq, Saddam Hussein. Aidha ameashiria namna ambavyo Iran inaendelea kuisaidia Qatar hivi sasa inapokabiliwa na mzingiro wa Saudi Arabia na waitifaki wake na kusema hiyo ni mifano ya namna ambayo Iran haiwaachi majirani zake wakati wa matatizo.
Ikumbukwe kuwa Jumatano iliyopita, Rais Hassan Rouhani akihutubu katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa alibainisha sera za kieneo na za kimataifa za Iran na kuwashilisha mpango wa 'Ubunifu wa Amani ya Hormouz' au 'Muungano wa Matumanini'. Rais Rouhani alitoa wito kwa nchi zote ambazo zinahusika kwa njia moja au nyingine na hali ya amani na usalama katika Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz kujiunga na muungano wa Jitihada za Amani katika Hormuz (Hormuz Peace Endeavor-HOPE).
Malengo na msingi wa Muungano wa Matumaini ni ishara kuwa, 'jitihada za juu kabisa' za Iran za kufikia utulivu, usalama na amani ya kudumu katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz ni mkamilisho wa sera za Jamhuri ya Kiislamu katika uga wa ujirani mwema, maelewano, uhusiano wa amani, ushirikiano baina ya nchi za eneo, kuheshimu mamlaka ya kujitawala kila nchi, kupambana na ugaidi na misimamo mikali, uhuru wa safari za meli za kibiashara, usalama wa nishati na uhuru wa kupita mafuta katika Lango Bahari la Hormuz.