Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran yatahadharisha kuhusu machafuko ya Iraq
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetangaza kuwa serikali na taifa la Iraq halitawaruhusu maadui na wageni kudumisha harakati zao na kutumia vibaya hali ya sasa nchini humo.
Taarifa iliyotolewa leo na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeeleza kusikitishwa na machafuko yanayoshuhudiwa hapa na pale katika miji kadhaa ya Iraq na kusisitiza kuwa: Serikali na taifa la Iraq wakishirikiana na makundi, vyama, watu mashuhuri hususan viongozi wakuu wa kidini na kisiasa wameingia kwenye medani kutuliza anga ya sasa na hawataruhusu kuendelea kwa harakati zinazosababisha hasara kwa taifa la Iraq na kuwapa wageni fursa ya kutumia vibaya hali hiyo.
Taarifa hiyo imetilia mkazo umuhimu wa matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) na udharura wa kufanyika vyema ipasavyo shughuli hiyo na imewataka wananchi wanaoshikamana na dini na maashiki wa Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw) wa Iran kuchelewesha safari yao ya kwenda Iraq kushiriki katika shughuli hiyo hadi hali itakapotulia na kusikiliza kwa makini tahadhari zinazotolewa na maafisa wa kisiasa na kiusalama.
Tangu Jumatatu iliyopita miji kadhaa ya Iraq ukiwemo wa Baghdad inashuhudia maandamano ya hapa na pale ya wananchi wanaosemeka kulalamikia matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa ajira. Vyombo vya habari vinasema kuwa watu 10 wameuawa mjini Baghdad na katika mkoa wa Dhi Qar katika makabiliano baina ya polisi wa kutuliza ghasia na waandamanaji.
Vilevile Waziri Mkuu wa Iraq, Adil Abdul Mahdi ametangaza marukufu ya kutembea watu na magari katika mji mkuu wa nchi hiyo, Baghdad kuanzia alfajiri ya leo Alkhamisi hadi hapo baadaye.