Iran: Tunakaribisha ushirikiano wa kuheshimiana baina yetu na Umoja wa Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56542-iran_tunakaribisha_ushirikiano_wa_kuheshimiana_baina_yetu_na_umoja_wa_ulaya
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inapokea vizuri ushirikiano wenye nia njema na wa kuheshimiana baina yake na Umoja wa Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 10, 2019 23:13 UTC
  • Iran: Tunakaribisha ushirikiano wa kuheshimiana baina yetu na Umoja wa Ulaya

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inapokea vizuri ushirikiano wenye nia njema na wa kuheshimiana baina yake na Umoja wa Ulaya.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Sayyid Abbas Mousavi amesema hayo ikiwa ni kuonesha hisia zake kuhusu kuteuliwa Josep Borrell kuwa mwakilishi mkuu wa Umoja wa Ulaya katika siasa za nje na masuala ya usalama ya umoja huo na kuongeza kwamba, ana matumaini kuwa Josep Borrell ataweza kusimama imara kukabiliana na siasa za kibeberu za Marekani za kujivutia kila kitu upande wake.

Aidha amesema, Iran inatumai kwamba mkuu huyo mpya wa sera za kigeni na kiusalama za Umoja wa Ulaya atakuwa imara pia mbele ya siasa za baadhi ya madola ya eneo la Asia Magharibi ambayo kwa siasa zao ghalati yamesababisha matatizo makubwa ya kidiplomasia.

Josep Borrell

 

Sayyid Abbas Mousavi amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatumai kwamba Bw. Josep Borrell ataendeleza msimamo ule ule aliokuwa nao Bi Federica Mogherini na kwamba Tehran inakaribisha ushirikiano wenye nia njema na wa kuheshimiana.

Ameongeza kuwa, wakati Bi Federica Mogherini alipokuwa ameshika nafasi hiyo alikuwa na msimamo mzuri na chanya katika uhusiano wa kimataifa na wa pande kadhaa na alikuwa na nafasi kubwa katika kufikiwa mapatano ya kimataifa ya nyuklia maarufu kwa jina la JCPOA.

Siku ya Jumatano, Bunge la Ulaya lilimteua rasmi Josep Borrell, Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani wa Uhispania kuwa Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya. Borell anatarajiwa kushika rasmi wadhifa huo mwanzoni mwa mwezi ujao wa Novemba, 2019 kuchukua nafasi ya Bi Federica Mogherini.