Rais Rouhani: Tuko tayari kuzungumza na Marekani iwapo itaondoa vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56621-rais_rouhani_tuko_tayari_kuzungumza_na_marekani_iwapo_itaondoa_vikwazo
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran iko tayari kuanzisha mazungumzo ya nyuklia na kundi la 5+1 ikiwemo Marekani, iwapo White House itaondoa vikwazo vya kidhulma ilivyoliwekea taifa la Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 14, 2019 11:50 UTC
  • Rais Rouhani: Tuko tayari kuzungumza na Marekani iwapo itaondoa vikwazo

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran iko tayari kuanzisha mazungumzo ya nyuklia na kundi la 5+1 ikiwemo Marekani, iwapo White House itaondoa vikwazo vya kidhulma ilivyoliwekea taifa la Iran.

Rais Rouhani amesema hayo jioni ya leo (Jumatatu) mbele ya waandishi wa habari wa ndani na nje hapa Tehran na kujibu swali kuhusu uwezekano wa kufanyika tena mazungumzo baina ya Iran na Marekani iwapo mchakato wa kumuuzulu Donald Trump utafanikiwa na rais mwingine kuingia madarakani huko Marekani, amesema, tatizo la Iran si kukaa katika mazungumzo na rais wa Marekani, bali lililo muhimu kwa Tehran ni iwapo maslahi ya taifa la Iran yatalindwa katika mazungumzo hayo au la.

Vile vile amesema, tabia za Trump zinalifanya suala la kuzungumza naye kuwa gumu sana. Leo Trump utamsikia amesema hivi, ukiamka kesho utamsikia amebadilisha msimamo wake. Leo utamsikia amekubali kkufanya mazungumzo na fulani, kesho atakanusha na kusema hakuna kabisa kitu kama hicho; na tatizo hilo haliko kwa Iran tu, bali liko kwa dunia nzima, ndiyo tabia ya Trump kwa viongozi wote duniani.  Vile vile amesema,  Iwapo vikwazo vitaondolewa kama tunavyotaka sisi, basi tutakuwa tayari kuwa sehemu ya mazungumzo katika fremu ya kundi la 5+1. 

Pande zilizofikia mapatano ya JCPOA

 

Trump ni mpinzani mkubwa wa mapatano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1 licha ya kwamba Marekani ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha makubaliano hayo muhimu yaliyo na baraka kamili za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mwezi Mei 2018, Trump aliitoa Marekani kwenye mapatano hayo bila ya sababu yoyote ya msingi na tangu wakati huo ameiwekea vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambavyo mwenyewe anajigamba kuwa ni vikubwa na vikali zaidi kuwahi kuwekwa dhidi ya nchi yoyote ile duniani.

Kujibu uvunjaji huo wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Tehran nayo ilitoa fursa ya mwaka mzima kwa nchi za Ulaya kuheshimu kivitendo makubaliano hayo, lakini zimeshindwa, hivyo Tehran nayo imeamua kupunguza hatua kwa hatua ahadi zake ndani ya JCPOA hadi pale nchi za Ulaya zitakapoheshimu kivitendo vipengee vyote vya makubaliano hayo.