Zarif: 'Uraibu wa vikwazo' wa Marekani unadhoofisha mahusiano ya kiuchumi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56806-zarif_'uraibu_wa_vikwazo'_wa_marekani_unadhoofisha_mahusiano_ya_kiuchumi
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uraibu wa Marekani wa kuziwekea vikwazo nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM na hata madola makubwa kama China na Russia unadhoofisha mahusiano ya kiuchumi duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 23, 2019 09:46 UTC
  • Zarif: 'Uraibu wa vikwazo' wa Marekani unadhoofisha mahusiano ya kiuchumi

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uraibu wa Marekani wa kuziwekea vikwazo nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM na hata madola makubwa kama China na Russia unadhoofisha mahusiano ya kiuchumi duniani.

Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo leo huko Baku mji mkuu wa Azerbaijan katika mkutano wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM na kusisitiza kwamba, hatua ya Marekani ya kuwa na uraibu wa kuyawekea vikwazo mataifa mengine mbali na kudhoofisha mahusiano ya kiimataifa inahatarisha pia uhai wa mamilioni ya watu kama ambavyo inakwamisha biashara kimataifa.

Dakta Muhammad Javad Zarif alipowasili Baku, Azerbaijan kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa NAM

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria udharura wa kuweko hatua za pamoja ulimwenguni za kukabiliana na ubeberu wa Marekani na akaongeza kusema kwamba, ni jambo la dharura na la haraka kwa jamii ya kimataifa kuwa na msimamo mmoja wa kuilazimisha Marekani iachane na hatua zake hatari na hivyo kuepusha kutokea maafa ya kibinadamu.

Dakta Zarif amesema, eneo la Asia Magharibi ndilo linalokumbwa na machungu zaidi kutokana na kusakamwa na chuki na uadui na kubainisha kwamba, Palestina kuwa na mamlaka yake ya kujitawala ni moja ya malengo muhimu kabisa ya Jumuiya ya NAM. Zarif ameashiria pia dhulma inayofanywa dhidi ya wananchi wa Yemen ambayo inaungwa mkono na Marekani na kueleza kuwa, hali hii imeshadidisha mizozo na ukosefu wa amani katika eneo hili.