Iran: Madikteta wasizungumzie kabisa haki za binadamu
Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amesema kuwa, ripoti mpya iliyotolewa na Javaid Rehman, ripota maalumu wa umoja huo imetolewa katika kuendeleza ugaidi wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya taifa la Iran na kwamba madikteta hawana nafasi ya kuzungumzia haki za binadamu nchini Iran.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Bw. Mohammad Hasani Nejad akisema hayo katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika jana na kuongeza kuwa, ripoti hiyo ya Javaid Rehman haina uhusiano wowote na haki za binamu, bali ni katika kuonesha hamaki za mabeberu na madikteta ambao wameshindwa katika njama zao zote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema, waistikbari na mabeberu hao leo hii hawawezi tena kuwaamulia Wairan nini cha kufanya na ndio maana ameamua kumalizia hamaki zao kwa kutoa ripoti za namna hiyo.
Mwakilishi huyo wa Iran katika Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, vitimbi na mashambulizi ya kila upande dhidi ya wananchi wa Iran yanafanyika kwa sababu tu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama kidete mbele ya ubeberu wa Marekani, ubaguzi wa Israel na kukaliwa kwa mabavu Palestina.
Jana Jumatano, Javaid Rehman, Muingereza mwenye asili ya Pakistan kwa mara nyingine alitoa ripoti inayokosoa sheria za Kiislamu za qisas (yaani kutekelezewa adhabu ya kifo mtu anayeua kwa makusudi na ikawa mawalii wa aliyeuliwa wametaka kulipiziwa kisasi mtu wao kwa kuuliwa aliyemuua). Javaid Rehman alikosoa pia adhabu ya kifo inayotolewa kwa wafanya magendo ya madawa ya kulevya nchini Iran na kudai eti sheria kama hizo ni uvunjaji wa haki za binadamu.