Ayatullah Movahedi-Kermani: Marekani ndiye muhusika mkuu wa matatizo ya Iraq
Khatibu wa Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran ameashiria matukio yanayoendelea hivi sasa nchini Iraq na kusisitiza kwamba tangu miaka 16 iliyopita, serikali ya Marekani ilikuwa ikiiba zaidi ya mapipa milioni moja ya mafuta ya nchi hiyo ya Kiarabu kwa kisingizio cha kufidia gharama za vita.
Ayatullah Mohammad Ali Movahedi-Kermani, amebainisha kwamba muhusika mkuu wa matatizo ya kiuchumi ya Iraq ni Marekani. Akibainisha kwamba adui anafuatilia kuona katika nchi za eneo hili kunapatikana fursa ili aweze kudhamini maslahi yake machafu, ameongeza kwamba, balozi wa Marekani nchini Iraq amekuwa akitangaza wazi uungaji mkono wake kwa machafuko yanayoendelea nchini humo sambamba na kuwataka polisi kutumia nguvu na ukandamizaji kuzima maandamano ya amani ya wananchi. Khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amesisitiza kwamba mirengo ya kisiasa ambayo inaungwa mkono na madola ya Magharibi, imehusika katika jinai mbalimbali mjini Karbala na Basra na kwamba raia wa Iraq wanatakiwa kujiweka mbali na mirengo hiyo.
Ayatullah Mohammad Ali Movahedi-Kermani, sambamba na kusisitizia umuhimu wa wananchi kufuatilia utatuzi wa matatizo ya kiuchumi yanayowakabili kwa njia za amani, amesema kuwa raia wa Iraq chini ya usimamizi wa maraajii wa kidini pamoja na serikali halali ya nchi hiyo, wanazo njia bora za utatuzi na uwezo wa kumaliza matatizo yanayowakabili kwa njia za amani. Akizungumzia matukio ya nchini Lebanon, Khatibu wa swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema kuwa msingi wa maandamano ya wananchi ni kitendo cha serikali kutozingatia matatizo ya kimaisha. Aidha amesisitiza kuwa, kujiuzulu Waziri Mkuu wa Lebanon kunaonyesha kwamba baadhi ya mirengo ya kisiasa nchini humo, inatumikia malengo machafu ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, Marekani na baadhi ya madola ya Kiarabu badala ya kuyapa umuhimu maslahi ya wananchi.