Watu wasiojulikana washambulia ubalozi mdogo wa Iran katika mji wa Karbala, Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i57045-watu_wasiojulikana_washambulia_ubalozi_mdogo_wa_iran_katika_mji_wa_karbala_iraq
Kanali ya televisheni ya Al-Alam imeripoti kuwa watu wasiojulikana wameshambulia ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji wa Karbala katikati mwa Iraq.
(last modified 2026-09-24T06:37:34+00:00 )
Nov 04, 2019 04:14 UTC
  • Watu wasiojulikana washambulia ubalozi mdogo wa Iran katika mji wa Karbala, Iraq

Kanali ya televisheni ya Al-Alam imeripoti kuwa watu wasiojulikana wameshambulia ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji wa Karbala katikati mwa Iraq.

Kwa mujibu wa Al-Alam, kwa kutumia kisingizio cha kulalamikia hali isiyoridhisha ya kiuchumi, kikundi kimoja cha watu kimeushambulia ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Karbala.

Duru za Iraq zimetangaza kuwa brigedi nne za vikosi vya usalama zimetumwa katika mji huo na kuwekwa kando kando ya jengo la ubalozi huo mdogo wa Iran ili kukabiliana na watu hao.

Katika siku za karibuni, wafanyahujuma wasiojulikana wamewashambulia mara kadhaa askari wa vikosi vya usalama pamoja na taasisi za serikali katika miji mbali mbali ya Iraq.

Maafisa wa serikali ya Baghdad wametangaza kuwa, hujuma na mashambulio hayo yanafanywa kwa madhumuni ya kuzusha fitna nchini humo.

Awali kabla ya hapo pia baadhi ya maafisa wa serikali ya Iraq walitoa hadharisho kuhusu njama zinazofanywa kwa kificho kwa lengo la kuharibu uhusiano wa kirafiki na kistratejia uliopo kati ya Iran na Iraq, ambao athari zake zimeshuhudiwa zaidi katika mapambano dhidi ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS).

Katika wiki za karibuni, mikoa kadhaa ya Iraq, imeshuhudia maandamano ya kulalamikia hali isiyoridhisha ya huduma za umma, kukosekana kwa ajira na ufisadi wa kiidara; lakini katika siku za karibuni maandamano hayo ya upinzani yamechukua mkondo wa fujo na machafuko na kusababisha makumi ya watu kuuawa na kujeruhiwa.

Maandamano ya upinzani nchini Iraq

Maandamano ya upinzani yangali yanaendelea nchini humo wakati katika kipindi cha mwezi mmoja sasa serikali ya Baghdad imeshawasilisha vifurushi vinne vya mapendekezo kwa lengo la kushughulikia matakwa ya waandamanaji.

Ushahidi uliopo unaonyesha kuwa maandamano ya nchini Iraq hayakutokana na vuguvugu la ndani ya nchi hiyo, bali kuibuka kwake kumechochewa na maajinabi.

Brigedi za Hizbullah ya Iraq zilitangaza hivi karibuni kuwa serikali ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zina mkono katika machafuko yanayotokea nchini Iraq kwa sababu hazipendezwi na sera za serikali ya nchi hiyo.

Mkuu wa Polisi katika mji wa Basra naye pia amebainisha kuwa, utawala wa Kizayuni, Saudi Arabia na Imarati zinafanya njama za kuvuruga utulivu na uthabiti nchini Iraq.../