Nov 06, 2019 03:09 UTC
  • Zarif: Nchi za Ulaya zifungamane na mapatano ya JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri wa Kiislamu ya Iran amezitaka nchi za Ulaya zifungamane na ahadi zao katika mapatano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA) .

Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter Jumanne usiku kabla ya Iran kuanza kuchukua 'Hatua ya Nne' ya kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA baada ya nchi za Ulaya kushindiwa kufungamana na mapatano hayo,  Mohammad Javad Zarif amesema: "Hatua ya Nne ya Iran katika kusitisha kwa muda utekelezwaji wa mojawapo ya vipengee vya JCPOA imeidhinishwa kwa mujibu wa ibara ya 36 ya mapatano hayo ya kimataifa, kama njia ya kujibu uamuzi wa Marekani na Troika ya Ulaya kukiuka mapatano hayo."

Zarif ameendelea kusema kuwa, utatuzi sahali wa kadhia hii ni kwa Umoja wa Ulaya na nchi tatu (troika) za Ulaya (Ujerumani, Ufaransa na Uingereza) kutekeleza ahadi zao katika JCPOA na zikifanya hivyo basi Iran itarejea katika mkondo wa kawaida.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu katika ujumbe huo pia ameambatanisha taswira ya mahojiano ya Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani mnamo Novemba 2018 na kukumbusha kuwa, Pompeo ndie chanzo cha Rais Donald Trump wa Marekani kuchukua maamuzi yasiyo sahihi kuhusu JCPOA.

Ikumbukwe kuwa, baada ya Marekani kuchukua hatua iliyo kinyume cha sheria na kujiondoa katika mapatano ya JCPOA mnamo Mei 8 2018, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza ziliahidi kukidhi maslahi ya kiuchumi ya Iran sambamba na kuyalinda mapatano hayo. Lakini nchi hizi hazijachukua hatua zozote za kivitendo za kukabiliana na uamuzi wa Marekani na zimetosheka tu na kutoa ahadi za maneneo.

Mei 8 2019, mwaka mmoja baada ya Marekani kuchukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na baada ya kubainika kuwa nchi za Ulaya hazijawasilisha njia za kivitendo za kufidia matatizo ya kiuchumi yaliyoibuka baada ya Marekani kujiondoa JCPOA, Iran ilitangaza hatua ya kwanza ya kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA kwa mujibu wa ibara za 26 na 36 katika mapatano hayo.

Hadi sasa Iran imechukua hatua 3 za kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA na leo Jumatano itachukua hatua ya 4.

Iran inasisitiza kuhusu kuendelea kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA lakini imesema inaweza kurejea haraka katika hali ya awali ya kutekeleza ahadi zake iwapo washirika wengine katika JCPOA watachukua hatua za kutekeza ahadi zao.

Kwa mujibu wa ibara za 26 na 36 za mapatano ya JCPOA, iwapo upande mmoja katika mapatano hayo utashindwa kutekeleza ahadi zake, Iran ina nayo pia ina haki ya kusitisha utekelezaji ahadi zake.

Tags