Nov 12, 2019 08:05 UTC
  • Zarif: EU haijachukua hatua yoyote ya maana ya kulinda JCPOA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezikosoa nchi za Ulaya kwa kuakhirisha ahadi zao na kufeli kufungamana na mapatano ya nyuklia ya JCPOA, huku zikiitaka Tehran ifungamane kikamilifu na makubaliano hayo.

Katika ujumbe alioutuma kwenye ukurasa wake wa Twitter, Mohammad Javad Zarif amezitaka nchi hizo za Ulaya zitoe ushahidi japo mmoja unaonesha kuwa zinafungamana na JCPOA katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.

Dakta Zarif ameandika: "Kwa wenzangu EU/E3 (Uingereza, Ufaransa na Ujerumani), eti mmefungamana kikamilifu na JCPOA? Nyinyi? Kweli?"

Zarif anasisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inatumia kipengee cha 36 kupunguza uwajibikaji wake kwenye JCPOA, baada ya nchi za Ulaya kushindwa kuchukua hatua za maana za kulinda maslahi ya Iran kwa mujibu wa vifungu vya mapatao hayo ya kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezitaka nchi za Ulaya kutupia jicho tena barua yake kwao ya Novemba 6 mwaka jana, ambapo alizionya kuwa Iran itachukua hatua ya kupunguza uwajibikaji wake kwa mujibu wa kipengee cha 36 cha JCPOA, baada ya Marekani kuanzisha wimbi la mashinikizo ya kiwango cha juu yaliyolenga karibu sekta zote za mafuta, fedha na usafiri za Iran.

Nchi za Ulaya zimekuwa zikishinikizwa na Marekani ama zijiondoe au zisifungamane na JCPOA

Amesema ni kinaya namna Jumuiya ya Kimataifa ya Mawasiliano ya Kibenki (SWIFT) ambayo inaziunganisha benki na taasisi nyingine za fedha kote duniani yenye makao makuu yake Ulaya, imesimamisha miamala yake ya kibenki ya karibu benki zote za Iran chini ya mashinikizo ya Marekani, huku EU ikitaka Iran ifungamane pekee kikamilifu na mapatano hayo.

Siku chache zilizopita,  Iran ilichukua uamuzi wa kuanza kutekeleza hatua yake ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, kufuatia hatua ya Marekani kukiuka mapatano hayo sambamba na ulegevu wa EU wa kutochukua hatua za kivitendo za kuyalinda mapatano hayo.

Tags