Iran yalaani uingiliaji kati wa Marekani katika masuala ya ndani ya Bolivia
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani uingiliaji kati wa Marekani katika masuala ya ndani ya Bolivia na mapinduzi baridi yaliyofanyika dhidi ya rais halali wa nchi hiyo.
Sayyid Abbas Mousavi amesema kuwa, hatua yoyote ya kubadilisha serikali kwa mabavu na kinyume cha sheria hususan kwa uingiliaji kati wa madola ya kigeni, inalaaniwa na haiwezi kukubaliwa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inaamini kuwa, mabadiliko ya aina yoyote yanapaswa kuakisi matakwa ya wananchi kupiitia masanduku ya kupigia kura na kwa mujibu wa sheria.
Mousavi ameongeza kuwa, anatarajia kwamba, wananchi na makundi ya kisiasa ya Bolivia yatatumia uwezo wa kisiasa na kisheria wa nchi yao kwa ajili ya kupata njia ya amani ya ufumbuzi wa hali ya sasa bila ya kutumia mabavu, mapigano na machafuko.
Rais Evo Morales wa Bolivia amelazimika kujiuzuluu kutokana na mashinikizo ya wapinzani wake wanaosaidiwa na kuungwa mkono na Marekani na jeshi la nchi hiyo. Morales amekubali kwenda uhamishoni nchini Mexico.