Rouhani: Wairani wana haki ya kuandamana bila kufanya fujo
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema wananchi wa taifa hili wana haki ya kufanya maandamano, lakini maandamano ya amani ni tofauti na uibuaji wa fujo na hali ya mchafukoge.
Rais Rouhani amesema hayo leo katika kikao cha Baraza la Mawaziri hapa Tehran na kuongeza kuwa, "Lengo la serikali la kukata ruzuku ya mafuta ni kuwasaidia wananchi wa matabaka ya kati na chini."
Amefafanua kuwa, "Ili kufanikisha hilo, serikali ina njia tatu tu za kufuata; ama kuongeza ushuru na kodi, au kuuza mafuta zaidi nje ya nchi au tupunguze ruzuku na kuzirejesha kwa wananchi wanaohitaji katika jamii."
Amesema uuzaji wa mafuta ya Iran nje ya nchi kwa sasa unakabiliwa na vizingiti vingi, na kwamba miaka minane iliyopita mapato ya mafuta ya Iran yalikuwa yanapindukia dola bilioni 110, lakini mambo ni tofauti hivi sasa kutokana na vikwazo.
Rais wa Iran amesema serikali yake haiwezi kuongeza ushuru kwa kiwango cha juu zaidi, na kwamba kulingana na hali ya sasa ya kiuchumi hapa nchini, ushuru huo unapaswa kuwa katika hali ya wastani.
Dakta Rouhani ameashiria kuhusu ongezeko la utumiaji wa mafuta hapa nchini na kubainisha kuwa, "Matumizi ya mafuta hapa nchini tangu mwishoni mwa mwaka jana hadi mapema mwaka huu yameongezeka kwa wastani wa asilimia 9.7, ambapo kwa siku tunatumia lita milioni 97 kwa siku; iwapo mkondo huu utaendelea, basi kufikia mwaka 1400 wa Kiirani (mwaka ujao 2020), tutalazimika kuanza kununua mafuta kutoka nje ya nchi."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei hapo jana aliunga mkono uamuzi wa mihimili mitatu mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) wa kukata ruzuku ya mafuta, jambo ambalo limepelekea bei ya bidhaa hiyo kuongezeka kwa karibu asilimia 50.