"Marekani inakusudia kuteka nyara maandamano ya amani ya Wairani"
Msemaji wa serikali ya Iran amesema Marekani inafanya juu chini ili kupotosha mkondo wa maandamano ya amani ya wananchi wa Iran wanaolalamikia ongezeko la bei ya petroli, lakini njama hizo zitagonga mwamba.
Ali Rabiei amesema hayo leo katika kikao na waandishi wa habari hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, "Utawala wa Marekani umeapa kuliweka taifa la Iran chini ya mashinikizo ya kiwango cha juu, lakini wanapoandamana kulalamikia athari za mashinikizo hayo, wanawahadaa eti tuko pamoja nanyi."
Amesema utawala wa Donald Trump haupaswi kujipendekeza kwa Wairani na kuwarubuni kuwa ina huruma nao na kuonyesha kuwa inawajali sana, katika hali ambayo serikali hiyo ya Washington inalifanyia taifa hili ugaidi wa kiuchumi.
Msemaji wa serikali ya Iran amebainisha kuwa, asilimia 75 ya wananchi wa Iran watastafidi na mpango wa serikali wa kukata ruzuku, kwani fedha hizo zitaelekezwa kwa familia na watu wenye vipato vya chini hapa nchini.
Hali kadhalika ameyatahadharisha makundi ya watu yanayochochewa kuibua ghasia hapa nchini na kueleza bayana kuwa, "Kila mmoja ana haki ya kufanya maandamano kwa amani, lakini hakuna mtu atakayeruhusiwa kushambulia biashara na mali za umma na za watu binafsi, au kutumia aina yoyote ya silaha, kwa kisingizio cha kulalamikia kuongezeka kwa bei ya petroli hapa nchini."
Aidha msemaji wa serikali ya Tehran amewahakikishia wananchi wa Iran kuwa huduma za intaneti zitarejea katika hali ya kawaida ndani ya siku chache zijazo.