Jeshi la kujitolea la Basiij katika mtazamo wa Kiongozi Muadhamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i57558-jeshi_la_kujitolea_la_basiij_katika_mtazamo_wa_kiongozi_muadhamu
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei Jumatano ya jana alihutubia hadhara kubwa ya maelfu ya wapiganaji wa kujitolea wa Basiij akieleza msingi wa kuundwa jeshi hilo kama taasisi ya kubadilisha vitisho na kuwa fursa. Vilevile ameeleza umuhimu wa nafasi ya Basiij katika nyanja mbalimbali za vita vya silaha na vita laini na vya kutumia teknolojia ya kisasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 28, 2019 14:12 UTC
  • Jeshi la kujitolea la Basiij katika mtazamo wa Kiongozi Muadhamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei Jumatano ya jana alihutubia hadhara kubwa ya maelfu ya wapiganaji wa kujitolea wa Basiij akieleza msingi wa kuundwa jeshi hilo kama taasisi ya kubadilisha vitisho na kuwa fursa. Vilevile ameeleza umuhimu wa nafasi ya Basiij katika nyanja mbalimbali za vita vya silaha na vita laini na vya kutumia teknolojia ya kisasa.

Ayatullah Khamenei ameashiria matukio ya hivi karibuni nchini Iran na machafuko yaliyoratibiwa katika baadhi ya maeneo ya Iran na kusema kuwa: "Maadui wametumia gharama kubwa kupanga njama hiyo na walikuwa wakisubiri fursa kwa ajili ya kuitekeleza kupitia njia ya kufanya uharibifu, mauaji na maovu mengine. Walidhani kwamba kadhia ya mafuta ya petroli ndiyo hiyo fursa iliyokuwa ikisubiriwa; hivyo waliingiza majeshi yao katika medani, lakini taifa la Iran limeangamiza njama hiyo..."  

Tajiriba na uzoefu wa miaka iliyopita vinaonesha kuwa, Marekani daima imekuwa ikitaka kudhoofisha utawala wa Kiislamu wa Iran na kusambaratisha umoja na mshikamano wa taifa la Iran kupitia njia ya kuzusha hitilafu na mifarakano ya ndani na inafanya kila iwezalo kuhakikisha kwamba Jamhuri ya Kiislamu inakumbwa na hitilafu za kisiasa na migawanyiko ya kijamii. Malengo haya ya Marekani yalishuhudiwa waziwazi katika machafuko ya hivi karibuni hapa nchini. 

Mtafiti wa sayansi ya siasa na mhadhiri wa chuo kikuu Sayyid Abdullah Mutawalliyan anasema: "Matokeo ya uchunguzi uliofanyika yanaonesha kuwa, timu ya kikosi kazi iketayarisha mradi mpya wa Marekani kwa ajili ya kuangusha utawala wa Jamhuri ya kiislamu wa Iran kupitia 'vita laini' (soft war) katika kalibu ya mpango wa "2020". Mpango huo unatekelezwa kupitia nyanja za kisiasa, kiusalama, kiuchumi na masuala ya kiutamaduni na kijamii."

Wapiganaji wa kujitolea wa Basiij

Wahusika wakuu wa njama na mpango huo wa Kimarekani wanaonekana vyema zaidi katika fitina na matukio miaka ya hivi karibuni na vilevile katika machafuko na ghasia za karibuni katika mitaa na maeneo ya baadhi ya maeneo ya Iran yaliyoibuliwa baada ya kuanza kutekelezwa mpango wa kubana matumizi ya petroli. Hata hivyo inatupasa kusema kuwa, moja ya sababu za kufeli mpango huo ni kutoelewa vyema nguvu za taifa la Iran. Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kwamba, katika kipindi chote cha miaka 40 iliyopita, utawala wa kibeberu wa Marekani umefanya kila kinachowezekana kwa ajili ya kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu lakini mti huo imara na madhubuti umeimarika zaidi na kuwa ngangari siku baada ya siku na kuwa kisiki mbele ya maadui zake.

Katika maneno yake muhimu kuhusiana na chanzo na sababu za njama hizo na mchango muhimu wa wananchi wa iran katika kuzima njama hiyo Ayatullah Ali Khamenei anasema: Utawala wa Kiislamu wa Iran unatokana na mafundisho ya Uislamu na unabeba bendera ya uadilifu na uhuru; na katika upande mwingine mfumo wa kibeberu kimsingi unapinga uhuru na uadilifu; kwa msingi huo mfumo wa Kiislamu wa Iran utaendelea kukabiliwa na vitisho vya mabeberu na kambi ya uistikbari.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Akieleza mifano ya upinzani wa kambi ya ubeberu hususan Marekani dhidi ya uhuru na uadilifu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Mfumo wa ubeberu daima umekuwa ukipinga kujitawala kwa mataifa mengine na kuyadhalilisha mataifa hayo. Mabeberu hao hawasiti kusema waziwazi nia yao katika uwanja huo kama inavyoshuhudiwa hii leo ambapo Marekani imetangaza waziwazi kwamba inepeleka majeshi huko kaskazini mwa Syria kwa ajili ya mafuta ya nchi hiyo. Mfano mwingine ni kuingia viongozi wa Marekani katika kambi ya majeshi yao huko Iraq bila ya idhini na wanapuuza serikali kuu ya Iraq.

Ukweli ni kwamba, Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran linaendelea kusimama kidete na kuwa macho mbele ya njama zote za maadui, na licha ya matatizo ya kiuchumi yaliyopo lakini halitatoa fursa kwa maadui zake.