Jibu kali la Iran kwa magaidi katika mipaka ya mashariki mwa nchi
Vyombo vya usalama katika mkoa wa Sistan Baluchestan, kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimetangaza habari ya kufichuliwa na kusambaratishwa magaidi wa kundi la Jeshi la Dhulma katika eneo hilo.
Idara kuu ya usalama wa eneo hilo ilitoa taarifa siku ya Jumapili ikitangaza kwamba magaidi wa kundi hilo walinaswa na askari usalama mara tu baada ya kuingia katikamkoa huo kwa madhumuni ya kutekeleza vitendo vya kigaidi. Taarifa hiyo imesema kuwa katika operesheni ya kuwanasa magaidi hao waliokuwa wamejizatiti kwa silaha tofauti na mada za kutengenezea mabomu, askari usalama wa Iran walifanikiwa kumuua kinara wa kundi hilo kwa jina la Ilyas Narui ambaye pia alikuwa akijulikana kwa jina bandia la Zubair.
Kinara huyo gaidi pia alikuwa na nafasi muhimu katika matukio mengine ya kigaidi katika ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yakiwemo yale yaliyotekelezwa katika mji wa Nikushahr ambapo askari wawili wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Sepah waliuawa shahidi, kulipuliwa basi na kuuawa askari 27 wa Sepah waliokuwa kwenye basi hilo katika mji wa Zahedan na kutegwa bomu la sauti katika kituo cha polisi katika mji huo.
Mara hii pia Ilyas Narui alikuwa na lengo la kujasusi na kuainisha vituo vingine vya kiusalama na kijeshi ambavyo vingelengwa na madaidi katika mji huo, lakini amepata jibu kali katika harakati zake hizo za kigaidi.
Siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kupambana vikali na ugaidi na kwa msingi huo huwa haisiti hata kidogo katika kutoa jibu kali dhidi ya wavamizi na magenge ya kigaidi yanayojaribu kuhatarisha usalama wa taifa la Iran. Katika mazingira tata ya hivi sasa, magaidi wanajaribu kila wanaloweza kuvuruga usalama na utulivu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakiwa wanafuatilia malengo mawili makuu.
La kwanza ni kujaribu kuonyesha kwamba hakuna utulivu na uthabiti wa kiusalama katika mipaka ya Iran.
La pili ni kujaribu kulipiza kisasi cha mapigo ambayo yametolewa na Iran kwa makundi ya kigaidi yanayodhaminiwa na nchi za eneo na za nje ya eneo hili.
Akizungumzia suala hilo hivi karibuni, Meja Jenerali Amir Hatami, Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko katika kiwango cha juu zaidi cha utayarifu wa kijeshi kwa lengo la kukabiliana vilivyo na kila aina ya vitisho vya adui. Amesema: Kushindwa hivi karibuni makundi ya kigaidi na kitakfiri katika eneo na hasa nchini Syria na Iran kumetoa pigo kubwa kwa Marekani na nchi nyingine zinazounga mkono makundi ya kigaidi katika eneo.
Kwa kuunga mkono Daesh na magaidi wengine wa kitakfiri, Marekani imedhihirisha wazi utambulisho wake ulio dhidi ya usalama katika eneo la Asia Magharibi, jambo ambalo limehatarisha usalama wa eneo hili lote.
Uzoefu unaonyesha kwamba ghasia na machafuko iwe ni katika eneo au kwenye mipaka ya nchi, yanahatarisha usalama wa eneo zima. Kwa kutilia maanani ukweli huo, Iran huwa haipotezi wakati katika kukabiliana na ugaidi na magaidi wanaohatarisha usalama wa mipaka yake, na kufikia sasa imethibitisha kivitendo kwamba inadhibiti vyema mipaka hiyo na kwamba haitawapa magaidi mwanya wowote wa kufanya chokochoko katika ardhi yake.
Akizungumzia suala hilo miezi kadhaa iliyopita katika mazungumzo yake na Imran Khan, Waziri Mkuu wa Pakistan aliyekuwa amefanya safari rasmi hapa nchini, Ayatullah Ali Khamanei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema: Makundi ya Kigaidi ambayo yanavuruga usalama wa mipaka yanapata misaada ya fedha na silaha kutoka kwa maadui na moja ya malengo ya harakati hizo zinazohatarisha usalama katika mipka ya Iran na Pakistan ni kuharibu uhusiano wa nchi mbili.
Kwa msingi huo, mapambano dhidi ya magaidi na kulindwa usalama wa mipaka ya nchi ni miongoni mwa masuala yanayosisitizwa sana mara kwa mara na Iran. Operesheni ngumu na kubwa ya kiusalama iliyotekelezwa siku ya Jumapili na walinda mipaka wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliotoa jibu kali kwa magaidi wa Jeshi la Dhulma katika mipaka ya mashariki mwa nchi, inaweza kutathminiwa katika mtazamo huo.