Wananchi wa Iran hawatasahau vikwazo vya kidhalimu vya Marekani katika siku hizi
Madai ya serikali ya Marekani kuhusiana na kutokuweko mbinyo na mipaka dhidi ya Iran kwa ajili ya kuingiza dawa na chakula ni urongo mkubwa.
Bijan Namdar Zanganeh, Waziri wa Mafuta wa Iran amesema hayo katika mahojiano aliyofaniywa na Kanali ya Televisheni ya Bloomberg ambayo yalirushwa jana Jumatatu ambapo alieleza kwamba, wananchi wa Iran hawatasahau vikwazo vya kidhalimu vya Marekani katika masiku haya.
Marekani inaendeleza vikwazo vyake vinavyokinzana na utu na ubinadamu dhidi ya Iran katika hali ambayo, wananchi wa taifa hili wanapitia kipindi kigumu cha kupambana na virusi vya Corona. Waziri Zanganeh sambamba na kubainisha kwamba, katika mazingira kama haya Marekani siyo tu kwamba, imekuwa ikichukua hatua dhidi ya serikali na wananchi wa Iran, ameongeza kuwa, serikali ya Washington imewawekea wananchi wa taifa hili vizingizti vingi na jambo hilo katika mustakabali linapaswa kuwasilishwa katika Mahakama ya Kimataifa.
Ugaidi wa kiuchumi wa Marekani umepelekea kuweko mashinikizo makubwa dhidi ya wananchi wa Iran. Mbali na vikwazo vya mafuta na kupanua wigo wa vikwazo vyake katika sekta ya viwanda, biashara na mabadilishano ya kifedha na kibenki, Marekani imefunga njia za Iran kununua dawa na suhula za kitiba. Sambamba na hatua hizo, Washington imeanzisha mchezo mchafu wa kisiasa wa kutaka kuonyesha kwamba, eti ni mfuasi wa wananchi wa taifa hili na inaguswa na matatizo wanayokabiliwa nayo.
Kwa bahati nzuri uwezo wa kielimu na teklojia ya tiba ya Iran na kwa kuwa kwake na maelfu ya madkatari wataalamu pamoja na wauguzi wenye kujali majukumu yao sambamba na vituo vya kisasa vya kufanyia vipimo vya udaktari, taifa hili la Kiislamu limeweza kujitosheleza katika nyanja nyingi. Miezi michache iliyopita pia, baada ya kuibuka virusi vya influenza vilivyokuwa vikiitishia jamii, Iran iliweza kwa mafanikio makubwa kuvidhibiti virusi hivyo.
Katika kukabiliana na virusi vya Corona pia, Iran inaona kuwa ina uwezo wa kuvishinda virusi hivi. Lakini kile ambacho kinasikitisha ni kutumiwa dawa na chakula kama silaha dhidi ya mataifa mengine hatua ambayo haina jina jingine ghairi ya jinai ‘jinai dhidi ya binadamu’. Marekani imekuwa ikitumia vikwazo kama wenzo wa sera zake za kigeni dhidi ya mataifa na serikali halali na hatua hiyo kwa hakika ni jinai dhidi ya binadamu.
David Cortright, Mkurugenzi wa Utafiti wa Kisiasa wa Kituo cha Kroc Kwa ajili ya Utafiti wa Amani ameandika katika makala: Baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza kuwa, anakusudia kutuma wanajeshi zaidi katika eneo la Asia Magharibi, wasiwasi kuhusiana na hatari ya kuibuka vita katika eneo hili uliongezeka. Lakini ukweli wa mambo ni kuwa, vita hivi ni vita vya kiuchumi ambavyo vimewalenga wananchi wa Iran na hivi sasa wananchi wa kawaida wanalipa gharama ya vikwazo hivi.
Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran ni kielelezo cha wazi cha jinai dhidi ya binadamu ambazo zinafanyika kupitia ‘ugaidi wa kiuchumi’.
Chambilecho Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ni kuwa, filihali ugaidi wa kitiba nao umeongezeka katika ugaidi wa kiuchumi wa Marekani.
Maafisa wa masuala ya afya, tiba na wauguzi wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Udaktari ya Iran wakisaidiwa na asasi nyingine, wote kwa pamoja wanafanya hima ya kupambana na virusi vya Corona na kuzuia visienee zaidi hapa nchini na katika eneo hili licha ya kuweko vikwazo vya Marekani. Licha ya kuwa katika uga wa afya na matibabu na hata katika utengenezaji dawa, Iran imepiga hatua na ina uwezo mkubwa wa kielimu na utaalamu katika uwanja huo kieneo, lakini hii haina maana kwamba, inapaswa kunyamazia kimya vitendo visivyo vya kibinadamu vinavyofanywa na serikali ya Washington.
Jamii ya kimataifa inataraji kuliona Shirika la Afya Duniani (WHO) likichukua hatua kali kukabiliana na vitisho na dhulma ambazo zinaharatisha usalama wa wanadamu. Hapana shaka kuwa, kukabiliana na virusi vya Corona ambavyo hadi sasa vimeenea katika nchi zaidi ya 100 duniani, kunahitajia ushirikiano mpana wa kimataifa. Hatua ya kimaonyesho ya Marekani katika uwanja huu inayofanyika kwa malengo ya kisiasa na kwa kutumia vibaya taabu na masaibu wanayopata wagonjwa na waathirika wa virusi hivi ni urongo mtupu ambao hatimaye utakuwa fedheha na aibu kwa viongozi wa Marekani.