Kuwa tayari kikamilifu Iran katika kudhibiti ugonjwa wa COVID-19
Richar Brennan, Mkuu wa Ujumbe wa Shirika la Afya Duniani (WHO) uliotumwa hapa Iran alisema jana Jumanne baada ya kutembelea vituo kadha vya matibabu mjini Tehran kwamba nguzo muhimu za kudhibiti magonjwa ya kuambukiza hususan virusi vya corona ni ushirikiano baina ya taasisi husika na wananchi na jambo hilo linaonekana kwa uwazi kabisa nchini Iran.
Brennan ameipongeza timu ya madaktari, wauguzi na watoa huduma wote za tiba nchini Iran na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo mkubwa wa kukabiliana na maradhi mbalimbali hasa ya kuambukiza na imeweza kuonesha uwezo wake huo kwa vizuri sana kila inapotokea migogoro na maafa tofauti.
Mkuu huyo wa Ujumbe wa Shirika la Afya Duniani (WHO) uliotumwa humu nchini kabla ya hapo alikuwa amesema kuwa, amevutiwa na maendeleo ya kielimu, ikhlasi na uchapaji kazi mzuri wa timu ya watoa huduma za tiba nchini Iran akisisitiza kuwa, nchi nyingine zilizokumbwa na virusi vya corona zinapaswa kutumia uzoefu wa Iran katika kupambana na virusi hivyo hatari.
Kwa upande wake, Dk Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Kama ilivyo kwa virusi vingine kama vile ugaidi, virusi vya ugonjwa wa COVID-19 navyo havifungwi na mipaka bali vinamkumba kila mtu na hakuna tofauti yoyote baina ya watu wa makabila na dini tofauti mbele vya virusi hivyo.
Virusi vya corona hivi sasa vimekuwa ni mgogoro wa dunia nzima. Virusi hivyo vimeenea sana kiasi kwamba Shirika la Afya Duniani WHO limetangaza hali ya hatari katika baadhi ya nchi. Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba ushirikiano wa taasisi zote na juhudi za kimatibabu ndiyo njia bora ya kuvidhibiti virusi hivyo.
Kwa upande wake, Dk Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Kituo cha Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari cha Wizara ya Afya ya Iran alisema jana Jumanne kwamba, hadi wakati anatangaza habari hiyo, watu 8042 walikuwa wamethibitishwa kukumbwa na virusi vya corona humu nchini na kuongeza kuwa, hadi wakati huo, watu 2731 kati ya hao walikuwa wamepona virusi hivyo nchini Iran na kuruhusiwa kurudi nyumbani. Pia alisema hadi wakati huo watu 291 walikuwa wamepoteza maisha kutokana na virusi hivyo humu nchini.
Hivi sasa kuna jitihada kubwa sana zinafanyika za kutafuta kinga na dawa ya kuzuia na pia kutibu virusi hivyo na kuna matumaini juhudi hizo zitazamaa matunda ya haraka na kuimarisha zaidi hali ya usalama wa kiafya katika jamii ya Iran na eneo hili lote kiujumla.
Katika mlolongo wa suala hili, kuna mambo mawili makuu ya kuzingatiwa. Mosi ni virusi vya corona vyenyewe na pili ni namna ya kukabiliana navyo. Vita dhidi ya virusi hivyo vitafanikiwa iwapo tu njia sahihi zitafutawa kama vile kurekebisha mtindo wa maisha katika jamii hasa masuala ya usafi na pia kurahisishwa upatikanaji wa vifaa vya tiba na kila suhula inayohitajika katika mapambano haya. Watu walioko mstari wa mbele katika vita hivyo ni madaktari na wauguzi ambao hivi sasa wanatumia uwepo wao wote kuhakikisha wanalinda usalama wa kiafya wa jamii. Kazi ya madaktari, wauguzi na watu wanaotoa huduma za matibabu nchini Iran ni kubwa na inayostahiki kushukuriwa na kupongezwa kiasi kwamba, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema, wananapambano hao walioko mstari wa mbele katika vita dhidi ya corona wanahesabiwa kuwa ni mashahidi katika njia ya kutoa huduma kwa jamii yao.
Dk Said Namaki, Waziri wa Afya wa Iran jana Jumanne aliyempendekezea Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu umuhimu wa kupewa cheo cha mashahidi watu wanaopoteza maisha katika juhudi za kupambana na virusi vya corona humu nchini, naye Ayatullah Sayyid Ali Khamenei aliafikiana na suala hilo.
Hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeelekeza juhudi zake zote katika kupambana na kuvishinda virusi vya corona, juhudi ambazo hadi hivi sasa zimezaa matunda mazuri na kupongezwa si tu na wananchi wa Iran, lakini pia na taasisi za kimataifa kama Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo limesema kwamba lina uhakika Iran itavishinda tu virusi hivyo.